Home » » Wavunaji miti Sao Hill walalamikia utaratibu wa utoaji vibali

Wavunaji miti Sao Hill walalamikia utaratibu wa utoaji vibali

WAVUNAJI wa miti katika Msitu wa Taifa wa Sao hill  uliopo Mufindi mkoani Iringa, wamelalamikia  utaratibu mpya wa utoaji wa vibali vya uvunaji wa miti katika msitu huo, kwa madai kuwa umelenga kuwadidimiza na siyo kuwakomboa kama malengo ya uanzishwaji wa shamba hilo yalivyokuwa hapo awali.

Wakilalamikia mgao huo katika kikao baina yao na kamati ya kudumu ya bunge  ardhi, maliasili na mazingira, msemaji wa wavunaji Bw. Dickson Lutelvele amesema utaratibu wa mgao wa mwaka huu umepungua kutoka Qubic mita 500 hadi kufikia 250, huku gharama ya usajili wa kibali ukipandishwa zaidi ya mara tatu, kutoka laki mbili hadi laki 7 na 82 elfu.

Aidha Lutevele amesema pia kodi ya mapato kwa kibali kimoja nayo imepandishwa mara mbili kutoka shilingi laki tatu hadi kufikia laki sita, jambo ambalo litawakwamisha kufanya shughuli hiyo katika msitu wa Saohill.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Bi. Evarista Kalalu na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ya Mufindi Bw. Peter Tweve wameiomba kamati hiyo kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo mapema, kabla halijaleta madhara kwa wananchi.
Hata hivyo mwenyekiti wa kamati hiyo ya kudumu ya ardhi, maliasili na mazingira, mh. Jemsy Lembeli amekiri kuona changamoto ziliyopo na kuwaomba wavunaji hao kuwa wavumilivu wakati yeye na kamati yake wakilifanyia kazi suala hilo, ikiwa pamoja na kulifikisha bungeni.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa