Home » » JESHI LA POLISI IRINGA LAWATAHADHARISHA WANAOJIPANGA KUFANYA UHALIFU NA MADEREVA WALEVI

JESHI LA POLISI IRINGA LAWATAHADHARISHA WANAOJIPANGA KUFANYA UHALIFU NA MADEREVA WALEVI




Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake leo.


Baadhi ya vifaa vya vinavyotumiwa na Jeshi la Polisi kupima mwendo kasi na kubaini madereva wanaoendesha wakiwa wamelewa.




Baadhi ya askari wa jeshi la Polisi na waandishi wa habari wakimsikiliza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi alipokuwa akiongea na waandishi wa habari.
 ========================================================================


Na Gustav Chahe

JESHI la Polisi Mkoani Iringa limewatahadharisha watu wanaojaribu kupanga mbinu za kusababisha uvunjifu wa amani katika siku ya kumkumbuka Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere itakayofanyika kitaifa mkoani Iringa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi alisema jeshi la polisi na vyombo vya usalama kwa ujumla wamejipanga vizuri kuweza kukabiliana na vitendo vya kihalifu.

Alisema idadi ya askari imeongezeka kwa kudhibiti vitendo ambavyo vinaweza kusababisha vurugu au uvunjifu wa amani.

Hata hivyo alisema hali ya usalama kwa Mkoa wa Iringa ni nzuri kutokana na ulinzi wa vyombo vya usalama na ulinzi shirikishi uliopo kila kona na kuwatakawale wenye nia ya kuvuruga amani kuingia katika Mkoa wasijaribu.

“Hali ya usalama kwa Mkoa wetu kwa ujumla ni nzuri, tumejipanga vizuri kwa ajili ya ulinzi wa wananchi na mali zao. Maaskari tupo wengi wenye sare na wasio na sare kwa hiyo wananchi wetu tunawaomba muwe na imani ya usalama” alisema Kamanda Mungi.

Mungi ametoa tahadhari pia kwa madereva wasiofuata sheria kuwa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na kwamba hakutakuwa na msamaha kwa yeyote anayevunja sheria barabarani.

“Wapo madereva vichwa maji wasiopenda kufuata sheria na wengine kuamua kuvunja sheria kwa makusudi tu. Wapo wasiopenda kutii amri ya askari barabarani wanaposimamishwa, hao watashughulikiwa bila huruma” alisema.

Kwamba wapo madereva wanaoendesha wakiwa wanaongea na simu jambo ambalo kiusalama na sheria za barabarani ni kosa na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa jeshi la polisi pindi wanapobaini dereva wa namna hiyo.

Amesema katika kukabiliana na vitendo vya usalama barabarani, jeshi la polisi lina vifaa maalum kubaini madereva wazembe na wavunjaji wa sheria na kwamba vifaa hivyo vinauwezo wa kuona mbali.

“Tuna vifaa vya kutosha kubaini madereva wanaoendesha wakiwa wamelewa. Dereva yeyote anapoingia Mkoa wa Iringa ajue hayupo salama kwa sababu tutampata tu hata akiwa mbali” alisema.



Misa ya kumkumbuka Baba wa Taifa itafanyika katika Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu (Kanisa la Kuu la Kiaskofu) Parokia ya Kihesa Jimbo Katoliki la Iringa ambayo inatarajiwa kuongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa ambapo baada ya Misa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete atakwenda kuhitimisha mbio za Mwenge na kuuzima ambazo zitafanyika kitaifa mkoni Iringa.
NA FRANCIS GODWIN 

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa