Na Eliasa Ally, Kilolo Iringa
KATIBU wa NEC, Itikadi na Uendezi wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Bw. Nape Nnauye, amesema vyama vya upinzani nchini,
vitaendelea kuwa na ndoto ya kushika dola kwani havina sifa hiyo zaidi kuvuruga
amani na kufanya vurugu.Alisema CCM inalaani vurugu zilizofanywa na upinzani
wiki iliyopita bungeni mjini Dodoma na kuwataka watambue dhamana waliyonayo
katika Bunge hilo kwa masilahi ya nchi, wapigakura.
Bw. Nnauye aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika
Kijiji cha Ruahambuyuni, Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa, wakati akizindua mbio
za bendera ya CCM inayokimbizwa mkoani humo na kuwaeleza wananchi utekelezaji
wa Ilani ya chama hicho.
Aliongeza kuwa, wabunge wa upinzani wamepewa
dhamana na wananchi ili kutetea masilahi yao si kupigana ngumi katika Ukumbi wa
Bunge na kumtaka Mbunge wa Mbeya Mjini, Bw. Joseph Mbilinyi (CHADEMA), kutafuta
ukumbi wa kupigania.
"Kama Bw. Mbilinyi anajiamini kwa kuwa na
uwezo wa kupigana, atafute ukumbi ili wananchi walipe kiingilio si kuharibu
sifa ya Ukumbi wa Bunge, lazima atambue thamani aliyonayo kwa wananchi.
" H a t a Mw e n y e k i t i w a CHADEMA
(Freeman Mbowe), atafute kazi nyingine ya kufanya kama ubunge umemshinda...
wananchi mnapaswa kufanya maamuzi magumu katika Uchaguzi Mkuu ujao kwa
kuwanyima kura wabunge wa upinzani ambao hawaendi bungeni kujadili masilahi
yao," alisema.
Alisema vyama vya upinzani vimegeuka kuwa vibaraka
wa wakoloni vikitumika kugombanisha wananchi, kuvuruga amani, umoja na
mshikamano uliopo.
Bw. Nnauye alisema, CCM itaendelea kutawala nchi,
kushika dola kwani hawapo tayari kuona Tanzania ikiongozwa na watu wasio na
chembe ya uadilifu na chanzo cha vurugu ambazo zinachangia vifo kwa baadhi ya
wananchi.
"CHADEMA wanapoanzisha vurugu, viongozi wao
huwa hawapatwi na madhara yoyote, matokeo yake husababisha vijana wasio na
hatia kupoteza maisha katika vurugu zao na wao hukimbia," alisema Bw.
Nnauye.
Alisema upinzani wamefanikiwa kuchukua baadhi ya
majimbo kwa sababu ya wana CCM wenyewe kwa wenyewe kutoelewana katika majimbo
husika, hivyo aliwataka kuwa na mshikamano ili kutotoa nafasi kwa upinzani
katika Uchaguzi Mkuu 2015.
"Viongozi wa CCM katika ngazi zote, wana haki
ya kuwabana kikamilifu Wakuu wa Wilaya ili watoe taarifa za maendeleo
yaliyofanywa na Serikali yao, akikataa tunamuomba aachie ngazi mwenyewe.
"Viongozi wazembe wasioweza kutekeleza Ilani ya CCM, kuendana na
kasi tunayotaka, hatumhitaji kwani wanatuangusha na kutufanya tueleweke vibaya
kwa wananchi," alisema.
Chanzo: Majira
0 comments:
Post a Comment