Na Oliver Richard, Iringa
IMEFAHAMIKA kuwa asilimia 67 ya watumishi wa
sekta ya afya katika Manispa ya Iringa hawana elimu na ujuzi wa huduma rafiki
kwa vijana, jambo linalosababisha kundi kubwa la vijana kukosa kupatiwa huduma
hiyo muhimu.
Hayo yalielezwa na Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto mkoani hapa, Mariam
Mohamed, katika maadhimisho ya Siku ya Afya ya Uzazi kwa Vijana mkoani hapa,
yaliyoandaliwa na Shirika la Tiba na Utafiti barani Afrika (AMREF).
Mariam alisema athari kwa vijana wa miaka 10-20 kwa ugonjwa wa ukimwi (VVU) ni
asilimia 14 kwa takwimu za mwaka 2010, ambapo asilimia 19 ya vijana hutumia
huduma rafiki ya afya ya uzazi kwa vijana.
Alisema asilimia 7 ya vijana wanaotumia vituo na kupewa ushauri nasaha na
upimaji wa virusi vya Ukimwi waligundulika kuwa na VVU, huku asilimia 67 ya
watumishi wa afya wa Manispaa ya Iringa wakiwa hawana ujuzi wa huduma rafiki ya
kutoa huduma hiyo kwa vijana.
Aidha kuhusu janga la Ukimwi Mkoa wa Iringa, Mariam alisema mkoa huo una
maambukizi kwa asilimia 15.7, huku taarifa za wajawazito wakiwa na maambukizi
kwa asilimia 14.6 katika takwimu za mwaka 2010.
Akitoa sababu zinazochangia tatizo la ugonjwa wa ukimwi mkoani Iringa, Mariam
alisema ni pamoja na kuendeleza mila na desturi ambapo asilimia 12.6 ya
maambukizi husababishwa na ukeketaji kwa wanawake, huku unyanyasaji wa kijinsia
ukiwa asilimia 35.
Alisema kwa upande wa wanaume wanaotahiriwa ni asilimia 34 pekee, huku asilimia
66 ya wanaume mkoani hapa wakiwa bado hawana desturi ya kutahiri, jambo
linalochangia tatizo la ugonjwa wa ukimwi.
Naye Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto, Sezalia Andrew, alisema kukosekana kwa
elimu ya afya ya uzazi kwa kundi hilo la vijana, kunasababisha ongezeko la
mimba kwa wasichana na hivyo kuwepo kwa matukio ya vifo vya uzazi.
Kwa upande wake, Dk. Elizabeth Mapella, Mratibu wa Afya ya Uzazi kutoka Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii, aliwataka vijana kujenga desturi ya kujisomea
vitabu ili kupata elimu mbalimbali, ikiwa pamoja na kufika katika vituo vya
afya kupata elimu ya afya ya uzazi.
Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Ipogolo, Shamira Lupola, alisema vijana wengi
wanashindwa kufika katika vituo vya afya kutokana na kutopewa fursa ya
kusikilizwa.
Winfrida Kiwone, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kihesa, alisema wazazi na
walimu waone umuhimu wa kushirikiana katika malezi ya watoto pasipo kutegeana,
kwani wote wana wajibu wa kumlea na kumlinda kijana asiingie katika janga la
ngono.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment