Na: Albert Sanga, Iringa.
Miezi kadhaa iliyopita kupitia redio TBC Taifa Ofisa mmoja wa wizara ya maliasili na utalii aliulizwa swali hili, “Je, inawezekana watu binafsi kuanzisha mashamba ya miti na kufanya biashara hii ya kuuza miti ya mbao nguzo ama karatasi?” Ofisa huyo alijibu hivi “..inaruhusiwa….hata mimi najilaumu kuwa miaka ile wakati tunapanda msitu wa serikali kule Mufindi mimi sikukumbuka kutafuta maeneo kwa wenyeji nikapanda miti.
Kama ningefanya hivyo nadhani leo na mimi ningekuwa milionea”. Mahojiano yale yamenipa hamasa ya kuileta makala hii wiki hii. Tangu mwanzoni mwa mwaka huu nimekuwa nikiandika makala za hamasa na ujenzi wa fikra kuhusu mitazamo yetu na uthubutu wa kufanikiwa kupitia biashara.
Nikiamini kuwa wengi mmeshajenga mitazamo chanya na utayari kuhusu biashara na uwekezaji; sasa nachukua hatua mpya. Hatua hii ni ya kuonesha na kuchambua tija (pay offs) za fursa mbalimbali za kibiashara.
Hadi kufika mwishoni mwa mwaka huu nimepanga kuwashirikisha fursa takribani kumi pamoja na utaratibu maalumu wa kuwasaidia wote watakaohitaji kuzichangamkia fursa hizo. Fursa nayoanza nayo leo ni hii ya kilimo cha miti. Nitakueleza kila kitu ikiwemo, hali ya biashara hiyo kwa sasa na miaka ijayo, gharama na hatua za kuanzisha biashara hiyo, usimamizi wa biashara hii.
Na mwisho kabisa nitakueleza jinsi nilivyojipanga kukusaidia wewe utimize ndoto yako ya kumiliki mashamba ya miti ikiwa utahitaji kufanya hivyo. Kilimo cha miti kimepata umaarufu wa ghafla miaka ya hivi karibuni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la mahitaji ya mazao ya miti na changamoto ya mazingira.
Katika Tanzania mkoa wa Iringa ni moja ya mikoa maarufu inayoongoza kwa misitu mikubwa ya kupandwa. Miti inatumika kwa mbao, nguzo za umeme, nguzo za kujengea pamoja na utengenezeaji wa karatasi.
Ukiacha mahitaji haya tuliyoyazoea hivi sasa kumeibuka fursa nyingine mpya ambapo mashirika ya kimazingira kutoka Magharibi yananunua hewa ukaa. Kwa maana hiyo unaweza kupanda shamba la miti halafu ukawa unakusanya dola kwa kuuza hewa ukaa wakati ukisubiri miti ikomae uvune mbao, nguzo ama miti ghafi ya kutengenezea karatasi.
Binafsi niliichangamkia biashara hii miaka mine iliyopita na ‘Im real serious with it’. Nimejiwekea lengo la kupanda ekari mia moja kila mwaka. Kilimo hiki cha miti ni uwekezaji wa muda wa kati na mrefu (middle& long term investments).
Kiutamaduni watanzania wengi huwa hawavutiwi na uwekezaji wa muda mrefu. Hata hivyo kama una mpango wa kuwa na baadae imara kiuchumi usikwepe kufikiria uwekezaji wa muda mrefu. Waingereza husema “Information is power”. Wengi hawajachangamkia fursa hii kwa kukosa taarifa tu.
Kazi yangu leo ni kukupa taarifa hizi za utajirisho. Ekari moja ya shamba inachukua wastani wa miti mia sita (600). Wastani wa chini wa mti mmoja kwa sasa uliokomaa vizuri ni shilingi elfu ishirini (20,000). Ina maana katika ekari moja ukiwa na miti iliyokomaa unakusanya jumla ya shilingi milioni kumi na mbili (12,000,000).
Fedha hiyo (kadirio la chini kabisa) utaipata ikiwa unaamua kuuza kwa bei ya jumla miti ikiwa shambani. Lakini kama ukiamua kupasua mbao wewe mwenyewe unaweza kuvuna mbao hadi za milioni ishirini na tano (25,000,000) kwa ekari moja.
Gharama ya kununua shamba tupu ni kati ya shilingi laki moja hadi laki tatu kutegemea na maeneo husika unayotaka ama kupata. Gharama za kuandaa shamba, kununua miche na kupanda ni kati ya shilingi laki tatu hadi nne.
Hii ina maana unaweza kumiliki ekari moja ya msitu wa miti kwa hadi shilingi laki nne tu! Kilimo cha miti ni rahisi sana kwa sababu ukishapanda hakihitaji uangalizi mkubwa sana na wala hauhitajiki uwe karibu na shamba/mradi muda wote.
Kuna kazi chache ambazo zinahitajika ukishapanda shamba lako. Mvua inyeshe ama isinyeshe mti wa mbao, nguzo ama karatasi ukishachipua huwa haufi kwani huendelea kutumia unyevu wa ardhini. Kazi namba moja unapokuwa umeshakamilisha upandaji wa miti kwenye shamba; ni kutengeneza njia za kuzuia moto walau mara moja kwa mwaka, kazi ya pili ni kufyekea miti inapokua walau kwa mwaka mara moja (prooning).
Gharama zote hizo yaani kutengeneza njia za moto, kufyekea na kulinda moto haizidi laki mbili kwa mwaka mzima. Miti hukomaa kuanzia miaka sita hadi kumi kutegemea na utunzaji unaoufanya.
Hii ina maana kuwa ukichukua shilingi laki mbili unazogharimia shamba kila mwaka ukazidisha mara miaka sita unapata shilingi milioni moja na laki mbili (1,200,000/=) au ukizidisha mara kumi unapata shilingi milioni mbili (2,000,000/=).
Kwa maana hii gharama za kuhudumia shamba la miti ekari moja kutoka kupandwa hadi kuvunwa ni kati ya shilingi milioni moja na laki mbili na milioni mbili. Ukichanganya na gharama ya kupata ardhi na kupanda miti yenyewe unapata kuwa gharama nzima hadi unavuna ni kati ya shilingi milioni milioni moja na laki sita kwa kadirio la chini. Hata hivyo nadhani wote tunafahamu kuwa ardhi ni rasilimali inayopanda thamani kila siku.
Vile vile tunatambua kuwa suala la mazingira ni tete kwa sasa na katika karne zijazo kama wataalamu wanavyotuthibitishia. Hii ina maana kuwa ukiwa na shamba la miti leo; thamani ya ardhi hiyo inazidi kupanda kila siku na miti uliyopanda inazidi kupanda thamani kila kukicha.
Jambo la uhakika ni kuwa hata kama bei ya miti, mbao, nguzo itayumba hutaweza kupoteza mtaji uliotumia na wala hutakosa kuzalisha faida kwa shamba utakalokuwa umemiliki, iwe ni eka moja, kumi, mia ama elfu moja. Mbali na hivyo unaweza ukaona, ahaa, miaka sita hadi kumi ni mingi mno; bado una nafasiya kupata faida hata ndani ya mwaka mmoja, miwili n.k. kwa kuamua kuuza miti ama pamoja na shamba kwa mtu mwingine.
Huenda hadi kufika hapa unaweza ukawa umeshavutiwa na biashara hii. Wengi wenu mnaweza kujiuliza maswali mkubwa mawili; “Ninatamani nifanye mradi huu lakini Iringa sikufahamu na hata kama nakufahamu nitaanzia wapi kupata hayo maeneo?”
Pili: Niko mbali na sina muda wa kushinda Iringa, Je, ni nani atanisaidia kupanda, kusimamia na kuendesha hayo mashamba? Kama si hayo maswali mawili hapo juu huenda ningekuwa nilishaandika makala hii tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Lakini nilisita kuandika fursa hii mapema pasipo kuwa na majibu ya maswali hayo kwa wasomaji. Leo nina majibu hayo.
Pia nikujulishe kuwa msimu wa kutafuta na kuandaa mashamba tunaanza Agosti-Oktoba na upandaji ni Novemba-Desemba hadi Januari kwa wanaokuwa wamechelewa sana. Sifa kubwa ya ujasiriamali ni kufanya huduma kwa watu wengine, yaani kutafuta mahitaji, shida, matatizo na matamanio yao na kuwatimizia. Kama alivyosema mfanyabiashara mmoja wa Kimarekani, Zig Ziglar “Utapata unachokitaka ikiwa utawasaidia watu wengine wengi kupata wanachokitaka”.
Katika kuwasaidia wengine ili wawekeze katika biashara hii ya mashamba ya miti ninaongozwa na mambo makubwa mawili ninayotaka kuona yakitimia. Mosi; mimi na wewe tuungane na serikali na dunia nzima katika kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kupanda miti mingi. Pili nataka nikusaidie wewe ambaye kila siku nimekuhamasisha ufikirie biashara na uwekezaji; uchukue hatua ya kuwekeza ili ujikwamue kiuchumi kwa kuvuna mamilioni.
Moja ya ndoto nilizonazo duniani ni kuzalisha na kuendeleza wafanyabiashara na wawekezaji wapya kwa maelfu hadi naingia kaburini. Huo ndio wito wangu duniani. Ili kutimiza ndoto yangu hiyo nimeweka utaratibu ufuatao utakaohakikisha kila mwenye ndoto, kiu na hamasiko la kuwekeza kwenye kilimo cha miti anafanikiwa. Kupitia mfumo wa biashara zangu nimeanzisha kitengo maalumu kijulikanacho kama Fresh Farms (T).
Kazi yangu kupitia kitengo hiki itakuwa ni kukupa ushauri wa kibiashara, kukutafutia maeneo ndani ya mkoa wa Iringa kwa ekari unazotaka, kukuandalia hayo mashamba, kukupandia hiyo miti na kusimamia utunzaji wa shamba katika hatua za awali na hata baadae.
Jisikie huru wakati wowote kuwasiliana nami kwa ufafanuzi na msaada wa fursa hii. Kwa kutumia sheria ya vijiji ya mwaka 1999 sheria na. 5, taratibu na tamaduni zote za wenyeji zinazohusiana na umilikaji ardhi nitahakikisha nakusaidia ili ndoto yako itimie.
Nadhani kwa utaratibu huu ipo siku nami naweza kusimama na kujivunia mazao ya watu waliokombolewa kivitendo kutokana na harakati zangu za kuelimisha watu kuhusu ujasiriamali, uchumi na biashara.
Hakuna sababu ya kulalamika wala kuwahofia wageni ya kwamba wanapora ardhi yetu ilhali sisi wenyewe wazawa hatuchangamki kuitumia ardhi yetu wenyewe kwa uzalishaji. Natamani watanzania wengi tuelekeze nguvu zetu katika uwekezaji wa kilimo na mazingira. Watanzania tunahitaji ushindi wa kiuchumi kupitia uwekezaji wa muda wa kati na mrefu!
Niandikie: stepwiseexpert@gmail.com.

0 comments:
Post a Comment