na Gustav Chahe, Iringa
MAUAJI ya
mwandishi wa kituo cha runinga cha Channel Ten, marehemu Daud Mwangosi,
aliyeuawa kwa kufyatuliwa bomu na polisi kijijini Nyololo mkoani Iringa,
yameendelea kuliandama jeshi hilo, ambapo wananchi mjini hapa nusura wampige
askari aliyevamia mkutano wa mbunge juzi.
Katika mkutano
huo wa mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA), uliofanyika
katika eneo la Soko Kuu mkabala na kituo cha polisi, askari mmoja alijitokeza
na kutaka kuwapiga wananchi kwa virungu bila sababu.
Wakati
Mchungaji Msigwa akiendelea kuhutubia, askari huyo alitokea kituoni hapo na
kwenda kutembeza virungu kwa watu, lakini kabla ya kuanza kazi yake, sauti za
wananchi zilipazwa zikisema, “Muacheni huyo ndiye atakayetuonyesha Mwangosi leo
hii.”
Wakati zogo
hilo likiendelea, kundi la vijana lilianza kumsogelea huku likisema: “Hatuogopi
mabomu wala bunduki za polisi.”
Purukushani
hizo, ziliwafanya askari wenzake kufika na kumvuta huku wakimkimbizia kituoni
kumnusuru na uamuzi waliotaka kuuchukua wananchi dhidi yake.
Tukio la kuuawa
kwa mwandishi huyo bado limevuta hisia za wananchi wengi ambapo shinikizo
linaelekezwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda,
likimtaka ajiuzulu kama sehemu ya uwajibikaji.
Akihutubia
wananchi hao, Mchungaji Msigwa, alilaani kitendo cha kuuawa kwa Mwangosi na
kusema kuwa hatatoa kauli yoyote isipokuwa atafanya kazi kwa vitendo na
kuhakikisha Kamanda Kamuhanda anaondoka.
“Hatuwezi
kulinda ujinga huu uendelee, mimi sitatoa tamko ila nitaanza kwa vitendo.
Hatuwezi kuuacha uozo huu. Kamuhanda lazima aondoke,” alisema.
Alilitaka jeshi
la polisi kumuogopa Mungu na kutenda haki badala ya kutii amri zinazohatarisha
usalama wa raia na kuwakatisha uhai.
“Nalaani
vitendo vyote vya jeshi la polisi vinavyohatarisha usalama wa raia. Na wale
wote wanaotoa amri kwa askari kwa ajili ya kuwapiga na kuwaua wananchi
washindwe na walegee kwa jina la aliyehai Yesu Kristo, Iringa hatukuzoea
matukio haya, sasa basi Kamuhanda lazima aondoke,” alisema Msigwa.
Aliwataka
wananchi wa Iringa kushiriki katika maandamano ya amani yatakayofanyika leo
kuanzia ofisi yake kuelekea katika ofisi ya Kamanda Kamuhanda kushinikiza
aondoke Iringa.
“Nyumbani kwetu
kuna nyoka, huyu nyoka lazima aondoke. Kila Ijumaa tutakuwa na maandamano ya
amani kumng’oa huyu nyoka na lazima polisi walinde maandamano hayo. Kamuhanda
ni nyoka lazima aondoke,” aliongeza.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment