Mwandishi wetu, Iringa
IDARA ya uvuvi katika halmashauri ya Wilaya ya Iringa imelazimika kufanya operesheni maalum ya kukamata vyavu haramu aina ya kokoro katika mialo mbalimbali ya bwawa la Mtera kwa upande wa wilaya za Mpwapwa na Chamwino Mkoani Dodoma baada taarifa za kuongezeka kwa uvuvi haramu kwa upande huo.
Afisa Uvuvi wa halmashauri ya wilaya ya Iringa, Raphael Fuvagwa amesema wameamua kuvuka mipaka hadi wilaya jirani kutokana kuongozeka kwa uvuvi haramu katika wilaya hizo huku idara za uvuvi katika wilaya hizo zikiwa hazichukua hatua za kukomesha hali hiyo.
Hata hivyo,Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya ya Chamwino, Daudi Mayeji amekanusha tuhuma zilizotolewa na Afisa uvuvi wa wilaya ya Iringa kwamba wilaya yao haifanyi lolote kuzuia uvuvi haramu katika bwawa hilo la Mtera kwa maelezo kuwa wamekuwa wakikamata zana nyingi haramu na kuteketeza mara kwa mara.
Wakati wilaya hizo zikitupiana mpira wa namna ya kupambana na uvuvi haramu, wavuvi kwa upande wao wameziomba mamlaka hizo badala ya kufikiria tu kushughulikia uvuvi haramu na kukusanya mapato pia zishughulikie maombi yao ya muda mrefu ya kutoa kibali cha kuwindwa kwa mamba na Viboka katika bwawa hilo kwa madai kuwa wameongezeka mno na mara nyingi wamekuwa wakikatisha maisha ya wavuvi kwenye bwawa hilo.
Katika operesheni hiyo ya siku mbili, jumla ya makokoro 25 yenye thamani ya Sh.milioni 25 yalikamatwa na kuteketezwa kwa moto jirani na kituo cha Polisi Mtera Iringa vijijini, mbele ya wawakilishi wa wavuvi pamoja na Mkuu wa kituo hicho.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment