Home » » WALIMU WAONDOLEWA HOFU UTEUZI WA MAKARANI WA SENSA

WALIMU WAONDOLEWA HOFU UTEUZI WA MAKARANI WA SENSA




Maelezo ya Picha: Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dk Christine Ishengoma wa tatu  kutoka kulia akiwa na baadhi ya viongozi wa mkoa na wilaya za Iringa wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wakufunzi wa sensa ngazi ya tarafa
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Dk Christine Ishengoma amesema taratibu na vigezo vitakavyotumika kuwapata makarani wa sense zitatangazwa wiki moja ijayo baada ya kupata miongozo kutoka  Ofisi ya Waziri Mkuu.
Taarifa ya Mkuu wa Mkoa huyo inaondoa ile hofu waliyokuwa nayo baadhi ya walimu watakaotumiwa katika shughuli hiyo kwamba uteuzi utafanywa kwa upendeleo
“Hili la taratibu na vigezo utaratibu wake utatangazwa baada ya wiki moja kuanzia sasa, kwahiyo wahusika wasiwe na wasiwasi hakutakuwa na upendeleo,” alisema.
Dk Ishengoma aliyasema hayo  alipokuwa akijibu swali kutoka kwa waandishi wa habari mara baada ya kufungua mafunzo ya siku moja ya wakufunzi wa sensa ya watu na makazi ngazi ya mkoa katika ukumbi wa Chuo Kikuu Ruaha, mjini hapa.
Katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa aliwahakikishia wakazi wa mkoa wa Iringa kwamba shughuli zao za kiuchumi na kijamii hazitaathiriwa na zoezi la sensa kwasababu litafanyika kwa siku saba kuanzia Agosti 26, mwaka huu.
“Ninawaomba wananchi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani wa sensa ili kupata taarifa muhimu na sahihi kwa ajili ya mipango endelevu ya maendeleo ya nchi yetu,” alisema.
Aliwataka viongozi wote wa vyama vya siasa, dini na serikali katika ngazi zote kwa ujumla watoe ushirikiano katika kuhamasisha na kuelimisha umma umuhimu wa kushirikiana na makarani wa sensa.
Hata hivyo akijibu moja ya maswali ya waandishi wa habari Mkuu wa Mkoa alikiri dodoso zitakazotumiwa kutokuwa na swali linahusu dini.
“Sensa haina dini, kwahiyo hakutakuwa na swali linalotaka kujua dini ya mtu, tunaomba viongozi wa dini mtusaidie pia kuwaelimisha waumini wenu kuhusu hilo,” alisema.
Awali Mratibu wa Sensa Mkoa wa Iringa, Fabian Fundi alisema mafunzo hayo yanashirikisha wakufunzi walioteuliwa kutoka halmashauri zote nne za mkoa wa Iringa.
Baada ya mafunzo hayo, Fundi alisema wakufunzi hao wataenda kutoa mafunzo hayo katika ngazi za tarafa zilizoko katika wilaya zao.
“Madhumuni ya mafunzo haya , yatawawezesha wakufunzi kufahamu taratibu zote zinazohusiana na kazi ya kuhesabu watu pamoja na kuwajengea uwezo wa kwenda kuwafundisha makarani na wasimamizi wa sensa katika ngazi ya tarafa,” alisema.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Getrude Mpaka alisema sense ya mwaka huu ni moja kati ya vipaumbele vya taifa na matokeo yake yatawezesha kupata takwimu muhimu za kufanya maamuzi sahihi na kupanga mipango endelevu ya maendeleo ya wananchi.
Chanzo: Frankleonard blog

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa