Home » » MASIKINI MWAKALEBELA, MAHAKAMA KUU YAITOSA RUFAA YA KESI YAKE YA RUSHWA, KAMA HAWATAKATA RUFANI MAHAKAMA YA RUFANI, SHAURI LAKE KUANZA KUSIKILIZWA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI MKOA WA IRINGA

MASIKINI MWAKALEBELA, MAHAKAMA KUU YAITOSA RUFAA YA KESI YAKE YA RUSHWA, KAMA HAWATAKATA RUFANI MAHAKAMA YA RUFANI, SHAURI LAKE KUANZA KUSIKILIZWA MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI MKOA WA IRINGA


ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Frederick Mwakalebela anatakiwa ajisalimishe Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) badala ya kusubiri kukamatwa baada ya vipengele alivyotumia kukata rufaa dhidi ya kesi yake ya rushwa wakati wa uchaguzi kutupiliwa mbali baada ya kuonekana havina nguvu mbele ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa.


Agosti mwaka 2010, Takukuru ilimfikisha mahakamani Mwakalebela kwa tuhuma za kujihusisha na utoaji wa rushwa wakati wa kampeni za kura za maoni za ubunge kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Iringa Mjini.

Katika kura hizo, Mwakalebela alimshinda kwa mbali aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Monica Mbega, hata hivyo alienguliwa kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huo baada ya Takukuru kumfikisha mahakamani kwa tuhuma hizo.

Katika kesi hiyo, Mwakalebela na mkewe Selina, kwa pamoja walikuwa wakituhumiwa kutoa hongo ya shilingi 100,000 kinyume cha sheria namba 15 (1) , (b) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambayo inasomwa kwa pamoja na kifungu cha 21 (1) , ( a) na 24 (8) ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010.

Mwezi Mei mwaka jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa, ilitupilia mbali kesi hiyo baada ya kusikiliza mapingamizi yaliyokuwa yamewekwa na Wakili wa mshitakiwa, Basil Mkwata na kuamuru upande wa jamuhuri kuifanyia mabadiliko hati hiyo kama wanataka kumfikisha tena mtuhumiwa huyo mahakamani.

Takukuru ikiwa katika mchakato wa kuifanyia mabadiliko hati ya mashitaka, wakili wa mshatkiwa alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa akiomba mahakama hiyo itolee uamuzi mapingamizi mengine ya kisheria ambayo Mahakama ya Hakimu Mkazi haikuyatolea uamuzi na mengine ikiyatolea uamuzi kimakosa.

Hoja ya kwanza ya wakili wa mshitakiwa iliyosikilizwa na Jaji aliyeendesha kesi hiyo jana, Rehema Mkuye ilidai, hati ya mashitaka iliyokuwa imaendaliwa na Jamuhuri haitengenezi kosa la jinai kisheria kwa kuwa makosa yote kama yalivyokuwa yametajwa kwenye hati hiyo yalikuwa yanakosa maneno.

Katika hoja hiyo, Jaji Mkuye alisema mahakama imepitia hoja za pande zote mbili na kuona hoja hiyo ingekuwa na nguvu kisheria kama mashahidi wangeitwa na kisha kutoa ushahidi wao.

“Kwa kuwa hilo bado halijafanyika Mahakama Kuu inatupilia mbali kigezo hicho cha rufaa,” alisema Jaji huyo.

Hoja ya pili ya rufaa hiyo ilieleza kwamba Kifungu cha 21 (1) (a) na Kifungu cha 24 (8) cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi Sheria No 6 ya mwaka 2010 ambacho mshitakiwa alikuwa ameshitakiwa nacho, hakikutengeneza kosa la jinai kisheria.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama iliona hoja zote zina nguvu kisheria lakini Jaji Mkuye alisema kulingana na kifungu cha 359 (2) cha sheria hiyo hiyo, hoja hiyo haikuwa imetolewa uamuzi wowote na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa hivyo haikutakiwa kukatiwa rufaa kwasababu hakukuwa na amri yoyote ya mahakama ya awali.

“Hivyo kwa kuwa rufaa iliyokuwa imekatwa na Wakili wa Mwakalebela ilikuwa na hoja mbili ambazo zote mahakama imezitupilia mbali, hivyo mahakama inatupilia mbali rufaa yote na amri ya mahakama ya Hakimu Mkazi ya kuifanyia marekebisho hati ya mashtaka na kumfikishe tena mtuhumiwa Mahakamani sasa itatekelezwa,” alisema jaji Mkuye.

Kaimu Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Iringa Stephen Mafipa alisema baadaye kwamba kikosi chake hakihitaji kumtafuta mtuhumiwa, bali atumie busara kujisalimisha ili afikishwe mahakamani.

Wakili wa mtuhumiwa alipofuatwa na vyombo vya habari ili atoe msimamo kwa niaba ya mteja wake  ikiwa ni pamoja na kama watakata rufaa katika Mahakama Kuu ya Rufani kupinga maamuzi ya Mahakama kuu, hakupatikana ofisini kwake.

Chanzo: Frankleonard Blog

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa