Home » » Manispaa yakazia karantini nyama ya nguruwe

Manispaa yakazia karantini nyama ya nguruwe


Mwandishi Wetu, Iringa
MANISPAA ya Iringa imeendelea kupiga karantini ya kuuzwa kwa nyama ya nguruwe, kutokana na kuongezeka kwa vifo vya mnyama huyo vinavyosababishwa na homa ya nguruwe.

 Ofisa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo Manispaa ya Iringa, Dk Nyenza Augustine, alisema msimamo wa kuendelea kuzuia uuzaji nyama hiyo, upo palepale kutokana na kujali afya za binadamu na kuokoa nguruwe ambao hawajaambukizwa.

Dk Augustine alisema takwimu za awali zilikuwa zinaonyesha nguruwe waliokufa ni 60, lakini idadi hiyo imeongezeka na kufikia 77 hali ambayo inawapa wasiwasi wa kuendelea kuenea kwa ugonjwa huo.
Alisema hatua hiyo imefikiwa kutokana na  baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, kwani wamekuwa wakichukua nguruwe kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa.  

“Tatizo wafanyabiashara wenyewe siyo waaminifu, wananunua nguruwe kwa bei nafuu kutoka maeneo mbalimbali na kuwaleta ilhali wakiwa na magonjwa,” alisema.

Kuhusu kukabiliana na ugonjwa huo, Dk Augustine alisema bado idara yake inaendelea kufuatilia kwa karibu, hasa wakati wa kusafisha mabanda ili kuzuia athari kwa nguruwe waliopo.

Pia, alitoa wito kwa watumiaji wa kitoweo hicho kuwa na subira mpaka idara yake itakapojiridhisha, kwani wakiendelea kupuuza marufuku hiyo wanahatarisha afya zao.

Mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe Manispaa ya Iringa, uliingia Mei 11 na kusababisha Idara ya Kilimo, Maendeleo ya Mifugo kufunga mabanda yote yanayouza nyama hiyo.
Chanzo: Mwananchi

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa