Home » » MH. MGIMWA KUHITIMISHA MIDAHALO YA WABUNGE WA IRINGA KESHO

MH. MGIMWA KUHITIMISHA MIDAHALO YA WABUNGE WA IRINGA KESHO


Na Francis Godwin Blog,Iringa

WAZIRI wa fedha na uchumi Dkt Wiliam Mgimwa kuhitimisha midahalo ya wabunge na wapiga kura kesho jumatatu jimbo la Kalenga.

Mratibu wa midahalo hiyo Raphael Mtitu ameueleza mtandao huu kuwa mdahalo huo kwa jimbo la Kalenga utafanyika kuanzia majira ya asubuhi katika ukumbi wa kijiji cha Ifunda kibaoni na kuwa midahalo hiyo ambayo ilianza kwa mbunge wa jimbo la Iringa mjini imefanyika pia katika jimbo la Kilolo na Isimani. 

Mtitu alisema kuwa midahalo hiyo ambayo inaendeshwa na asasi za kiraia nchini na kuratibiwa na asasi ya ICISO imekuwa na mwamko mkubwa kwa wananchi kutaka kujua maendeleo ya majimbo yao huku wabunge wakitumia nafasi hiyo kueleza kile walichokifanya.

Hata hivyo aliwataka wananchi wa jimbo la Kalenga kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mdahalo huo ambao umelenga kuwakutanisha na mbunge wao ili mbunge kuweza kueleza kile alichokifanya na wananchi kuhoji ama kupatiwa ufafanuzi juu ya ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni ama mambo mbali mbali ya kimaendeleo ambayo yanafanyika ama hayafanyiki katika jimbo husika.

Mtitu alisema kuwa mtandao huo umeandaliwa na mashirika yasiyo ya Kiserikali katika Mkoa wa Iringa ( Iringa Civil Society Organization [ICISO- UMBRELLA]) kwa kushirikiana na mitandao ya AZAKI ya Halmashauri ya manispaa ya Iringa (Iringa Municipal Civil Society Organization – IMUCISO), Iringa vijijini (Iringa Rural Non-Governmental Organization – IRUNGO) na Kilolo (Kilolo District Non-Governmental Organzations Umbrella – KIDINGOU),

Pia alisema kuwa midahalo hiyo ililenga kuwaongezea uelewa wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii na kiuchumi yanayohusu ili waweze kumiliki michakato ya kuleta maendeleo yao badala ya kutegemea serikali na wahisani pekee.

Hata hivyo aliwataka wabunge wote kushiriki katika midahalo hiyo inayowapa fursa wapiga kura kuongea na mwakilishi wao Mwenyekiti wa Halmashauri moja kwa moja ili waweze kutoa dukuduku zao na kuuliza maswali na kujibiwa papo hapo

· Wananchi wapate kujua shughuli alizozifanya/atakazofanya sehemu mbalimbali ndani ya jimbo/wilaya pamoja na utekelezaji wa ilania ya chama chake, ahadi za Rais pamoja na viongozi wengine wa kitaifa

Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika midahalo hiyo kwenye jimbo la Iringa mjini linaloongozwa na mchungaji Peter Msigwa (Chadema) jimbo la Kilolo linaloongozwa na mbunge Profesa Peter Msolla na jimbo la Isimani linaloongozwa na mbunge Wiliam Lukuvi ambaye ni waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu sera na uratibu wa bunge ,alisema kumekuwepo na mafanikio makubwa zaidi kwa wananchi kujitokeza kwa wingi na kujua mipango na mikakati ya maendeleo katika jimbo lao.

Mtitu alisema midahalo hiyo haifungamani na itikadi ya chama chochote cha kisiasa na kuwa hata wananchi wanaofika katika midahalo hiyo hawapaswi kuja na bendera wala sare ya chama chochote cha kisiasa.

0 comments:

 
Blogs za Mikoa
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa