Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKOA wa Iringa unaelezwa kujitosheleza kwa chakula kutokana na mavuno
ya tani 1,291,070 za nafaka, mikunde na mizizi kwa msimu wa mwaka
2014/15.
Hayo yalielezwa hivi karibuni na Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na
Sekta za Uzalishaji, Fikira Kisimba wakati akitoa taarifa ya mandeleo ya
kilimo kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana kwa Kamati ya Ushauri ya
Mkoa. Kisimba alisema nafaka pekee zilizovunwa katika msimu huo ni tani
963,981, mikunde tani 135,352 na mizizi ni tani 191,737.
Kwa mujibu wake, mkoa huu ulihitaji tani 346,989 za nafaka na mikunde
ili kutosheleza wakazi wake kwa mwaka mzima, hivyo kutokana na mavuno
hayo, unajitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ya tani 651,691 za
nafaka.
“Lakini pamoja na kuwa na ziada ya chakula, yapo baadhi ya maeneo
katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa na Kilolo yenye upungufu wa
chakula,”alisema na kuyataja maeneo hayo kuwa ni tarafa za Isimani,
Pawaga, Idodi, Mahenge na Mazombe.
Katibu Tawala Msaidizi huyo alieleza sababu za upungufu huo wa
chakula katika maeneo hayo kuwa ni ukame uliosababisha mavuno chini ya
asilimia 30.
Akielezea jitihada zilizofanywa na mkoa, Kisimba alizitaja kuwa ni
kupeleka maombi ya chakula katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa
pamoja na kuomba kibali cha wafanyabiashara wenye mashine za kusaga
kwenye maeneo ya waathirika ili kununua mahindi kutoka kwa Wakala wa
Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA - Makambako) ili wauze unga kwa
waathirika wa njaa kwa bei nafuu.
Agosti mwaka jana, mkoa ulipata kibali cha kununua tani 100 za mahindi kwa ajili ya mkoa huu.
“Novemba mwaka jana tulipata kibali cha kuchukua tani 400 za mahindi
ambapo, tani 320 zilikuwa ni za Halmashauri ya wilaya ya Iringa na tani
80 kwa ajili ya Halmashauri ya wilaya ya kilolo. Desemba mwaka huo mkoa
ulipata pia kibali cha kununua tani 350 za mahindi ambapo 200 zilikuwa
ni za Halmashauri ya wilaya ya Iringa na tani 150 za Halmashauri ya
wilaya ya Kilolo,” alisema Kisimba.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment