KIKUNDI cha wakulima wa kijiji cha Mangalali, Iringa vijijini
kimeongeza uzalishaji wa mahindi kutoka gunia nane hadi 20 kwa ekari,
baada ya kupata mafunzo ya kanuni bora za hifadhi ya mazao.
Mafunzo hayo yamewawezesha kupunguza upotevu wa nafaka katika
mchakato wa kuvuna hadi kuhifadhi. Mwenyekiti wa kikundi hicho, Emelita
Singaile, alisema kikundi hicho chenye wanachama 184 wenye wastani wa
ekari tano kwa kila mmoja, kilianzishwa mwaka 2003 kikiwa na wanachama
45 na sasa kinanufaika na kuona matunda ya kilimo kutokana na kusimamia
kanuni za kilimo.
Singile alisema mafunzo hayo kupitia mradi husishi wa kupunguza
upotevu wa nafaka katika mnyororo wa thamani wa zao la mahindi
unaoratibiwa na taasisi ya maendeleo mijini na vijijini (Rudi),
yalifadhiliwa na taasisi ya Mapinduzi ya Kijani Barani Afrika (AGRA)
inayosaidiwa na Taasisi ya Rockefeller Foundation ya Marekani.
Akitoa taarifa kwa wawakilishi wa Rockefeller Foundation
waliowatembelea wakulima hao hivi karibuni, Singaile alisema kwa kupitia
mradi huo wamepata pia mafunzo ya kilimo bora cha mahindi na ya
matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo.
“Tunavuna kwa kutumia maturubai yanayosaidia kupunguza uwezekano wa
mavuno kupata maambukizi ya sumu kuvu (aflatoxin) pamoja na punje
kupotea,” alisema.
Alisema mahindi wanayovuna, wanahifadhi kwa kutumia mifuko
isiyoingiza hewa (PICS na AgroZ bags), Kihenge cha Chuma (metal silo) na
kifukofuko (Cacoon).
Meneja wa Rudi, Allan Ngakonda alisema teknolojia hizo za uhifadhi
kwa pamoja zinalifanya zao hilo kuwa katika hali ya usalama kwa muda
mrefu zaidi bila kutumia kemikali zozote na hivyo kusaidia kulinda afya
za walaji.
Alisema kabla ya mradi kuja na matumizi ya teknolojia hizo, wakulima
walikuwa wanapoteza asilimia kati ya 25 na 40 ya mazao wanayovuna.
0 comments:
Post a Comment