Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
TEMBO
wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya
Iringa Vijijini, watafungwa kifaa maalumu cha kufuatilia mwenendo wa
wanyama hao ambao wapo katika kasi kubwa ya kutaka kutoweka kwenye
ramani za hifadhi.
Hatua hiyo inatokana na ujangili unaoendelea
ambapo vifaa hivyo vinakuwa kwenye harakati za ziada za serikali na
wadau wake za kuwanusuru wanyama hao na majangili wa meno yake.
Mpango
huo utakaotumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya satelaiti ya
utambuzi wa jiografia ya maeneo (GPS) na kompyuta utatekelezwa kupitia
Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania
(SPANEST) ili kuhakikisha kuwa kundi la wanyama jamii ya tembo
wanalindwa na kuendelea kuishi ili vizazi vijavyo viione rasilimali hiyo
muhimu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mratibu wa
SPANEST, Godwell Olle Meingíataki kwenye ukumbi wa ofisi ya VETA Mkoa wa
Iringa alisema kuwa, wako katika hatua za mwisho za utekelezaji wa
mpango huo na kuongeza kuwa hatua ya kuwafunga tembo wote itakuwa
imetafutiwa ufumbuzi mkubwa ambapo kila tembo atajulikana kwenye mtandao
huo wa kompyuta.
"Kwa kupitia mpango huo tutakaoutekeleza ndani ya
hifadhi zetu tembo, viongozi wa makundi ya tembo watafungwa kifaa
maalumu shingoni kitakachokuwa kinatoa taarifa za mwenendo wao katika
kila eneo watakalokuwepo ndani na nje ya hifadhi na tunahakika kupitia
mpango huu tutawanusuru wanyama hawa," alisema Godwell.
Aliongeza
kuwa, kwa kupitia kifaa hicho askari wa wanyamapori watakabiliana
kirahisi na majangili wa meno ya tembo katika azma ile ile ya kunusuru
kiumbe hicho kinacholiingizia Taifa mapato makubwa ya kigeni na kuwa
kila kundi la tembo kwa sasa litakuwa linalindwa kwa umakini zaidi kwa
kuwa litajulikana kiurahisi maeneo lilipo.
Alisema kuwa, kwa kupitia
mradi wa SPANEST, Februari mwaka huu, Hifadhi ya Ruaha ilipata msaada
wa vitendea kazi mbalimbali yakiwemo magari mawili ya doria yaliyotolewa
na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP) na kuongeza kuwa
mpango huo wa kutoa msaada umewezesha zaidi kuimarika kwa ulinzi ndani
ya hifadhi hiyo.
Alisema, vifaa vya mawasiliano vitafungwa katika
magari hayo na mengine ya hifadhi hiyo ili kuwezesha mawasiliano na
uchukuaji wa hatua za haraka pale zitakapotokea taarifa tata kuhusiana
na tembo hao ambapo Oktoba hadi Novemba mwaka jana, Wizara ya Maliasili
na Utalii ilifanya sensa ili kuiwezesha serikali kutambua hali ya
rasilimali ya wanyamapori ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa.
Alisema
kuwa, katika taarifa ya wizara hiyo inaonesha kwa kushirikiana na
wataalamu wa ndani na nje ya nchi walifanya sensa katika maeneo ya mfumo
wa ikolojia yenye tembo wengi ya Selous, Mikumi, Ruaha na Rungwa na
kuwa matokeo hayo yanaonesha mfumo wa ikolojia wa Ruaha una tembo wengi
kuliko hifadhi nyingine nchini ukiwa na tembo wapatao 20,090.
Matokeo
hayo yanaonesha kwamba mfumo wa Ikolojia wa Selous-Mikumi kwa sasa una
tembo wapatao 13,084 wakati mwaka 1976 kulikuwa na tembo 109,419 ambapo,
Meingíataki alisema juhudi za makusudi zinazofanywa na serikali ikiwa
ni pamoja na kuimarisha doria na operesheni maalum mbalimbali zitasaidia
kupunguza wimbi la ujangili.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment