Home » » NI CCM KALENGA

NI CCM KALENGA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

MATOKEO ya awali katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, yanaonesha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimepata ushindi wa kishindo katika kata 11 kati ya 13, ambapo idadi ya vituo vya kupigia kura vilikuwa 200.
Kata hizo ni Lumuri, Kalenga, Kiwere, Mgama, Ifunda, Magulilwa, Nzihi, Ulanda, Wasa, Lyangungwe na Mseke ambapo kata za Maboga na Luhota matokeo yake hadi tunakwenda mtamboni yalikuwa hayajatangazwa.
Kata ya Ifunda inadaiwa kuwa ngome ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kilifunga kampeni zake katika kata hiyo.
Dosari zilizojitokeza katika uchaguzi huo ni pamoja na baadhi ya wapigakura waliokuwa na shahada za kura, kukuta majina yao hayapo kwenye vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo, mmoja wa waangalizi wa uchaguzi huo kutoka Makao Makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), aliyefahamika kwa jina la Kaijage, alisema wote ambao majina yao hayajaonekana lakini wana shahada, wajaze fomu maalumu na kuruhusiwa kupiga kura.
Matokeo ya awali kwenye vituo, Ofisi ya Kijiji Tagamenda CCM-64, CHADEMA-53, CHAUSTA-0, Ofisi ya Kijiji Ugwachana, ccm- 91-CHADEMA-31, CHAUSTA-0,, Ofisi ya Kijiji Tanangozi 1, CCM- 86, CHADEMA-46, CHAUSTA-2.
 Tanangozi 2, CCM-79, CHADEMA-28, CHAUSTA-0, Shule ya Msingi Mtivila, CCM-83, CHADEMA-17, CHAUSTA-1, Tosa 1, CCM-98, CHADEMA-20- CHAUSTA-0, Ipamba 2, CCM-104, CHADEMA-10, CHAUSTA-0.
Isakulilo, CCM-83 , CHADEMA-8, CHAUSTA-0, Kilindi A, CCM-69, CHADEMA-23, CHAUSTA-0, Ofisi ya Kijiji (Kilindi), CCM-117, CHADEMA-53, CHAUSTA-0, Zahanati CCM 117, CHADEMA-67, CHAUSTA-0.
Kata ya Ifunda, Kivavali A, CCM-99, CHADEMA-19, CHAUSTA-0, Kivalali B, CCM-109, CHADEMA-14, CHAUSTA-0, Muwimbi CCM-164, CHADEMA-22, CHAUSTA-0, Mahanzi CCM-130, CHADEMA-46, CHAUSTA-0.
Ikungwe A, CCM-131, CHADEMA-23, CHAUSTA-0, Ikungwe B, CCM-216, CHADEMA-13, CHAUSTA-0, Magunga CCM-184, CHADEMA-4, CHAUSTA-1, Wasa CCM-149, CHADEMA-15, CHAUSTA-0, Usengelidate CCM-260, CHADEMA-46, CHAUSTA-0.
Kutokana na matokeo hayo ya awali, wafuasi wa CCM walianza kushangilia ushindi kwenye maeneo mbalimbali ya jimbo hilo wakiwa wameshika vipande vya miti na kucheza ngoma.
Utulivu Kalenga
Wakazi wa jimbo hilo, walijitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura ambapo hali ya amani na utulivu, ilitawala katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja asubuhi ambapo misururu mirefu ilianza kuonekana muda mfupi baada ya kazi ya kupiga kura kuanza.
Miongoni mwa vituo vilivyokuwa na idadi kubwa ya wapigakura ni vile vilivyopo kwenye kata ya Kalenga Mjini, Kata ya Kalenga na Mangalila vilivyo kwenye Kata ya Ulanda.
Katika Kata ya Maboga, vituo vyote vya kupigia kura vilifunguliwa mapema ambapo akizungumza na Majira baada ya kupiga kura, Bw. Onesmo Makasi, mkazi wa Mangalila, alisema awali alidhani uchaguzi huo utagubikwa na vurugu kutokana na kauli zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya wanasiasa.
"Nimepiga kura kwa amani na utulivu, kutokana na utaratibu huu naamini mshindi atatangazwa mapema," alisema.
Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Zaina Konzi aliipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa amani.
Ulinzi uliimarishwa katika vituo vyote vya kupigia kura ambapo askari mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake kwenye Kituo cha Kalenga A na B, alisema wamejipanga vizuri kulinda amani na kudhibitio viashiria vya vurugu.
Helikopta ya Chadema
CHADEMA waliitumia helkopta yao kuzunguka katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo. Baadhi ya kata ambazo zilifikiwa na helikopta hiyo ni Kalenga, Nzihi, Ifunda na Wasa.
Jeshi la Polisi mkoani humo, lilizuia matumizi ya helikopta siku ya jana ili kuwawezesha wananchi kupiga kura kwa utulivu lakini CHADEMA waliitumia kwa kutoa nembo ya chama ili kutokiuka sheria na kanuni za uchaguzi.
Kauli za vitisho
Kabla ya uchaguzi huo, kauli mbalimbali za vitisho zilikuwa zikitolewa na baadhi ya wanasiasa walipokuwa kwenye mikutano ya kampeni na kuonekana kuwatia hofu wananchi.
Kuna zilizodai kuna vijana waliofichwa porini kwa ajili ya kuzuia watu wasiende kupiga kura hivyo kusababisha hofu kwa baadhi ya wananchi wakihofia usalama wa maisha yao.
 Baadhi ya wananchi waliamini uchaguzi huo ungegubikwa na vurugu kutokana na kauli za wanasiasa hao ikiwemo ya baadhi ya makundi ya vijana kuingizwa jimboni humo.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ramadhan Mungi alisema polisi wamejipanga kukabiliana na kila aina ya hila zinazoweza kuvuruga uchaguzi huo.
Kauli hiyo imesaidia kuimarisha hali ya amani jimboni humo ambapo wapigakura walipiga kura zao bila vitisho.
Vyama vitatu vilishiriki katika uchaguzi huo ambavyo ni CCM, CHADEMA na CHAUSTA. Mgombea wa CCM ni Bw. Mgimwa, CHADEMA alikuwa, Bi. Grace Tendega na CHAUSTA, Bw. Richard Minja.
Hadi tunakwenda mtamboni, NEC ilikuwa haijatangaza rasmi matokeo hayo wala kumtangaza mbunge mteule wa jimbo hilo.

Chanzo:Majira

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa