ONSPOT MAGAZINE

ONSPOT MAGAZINE

MGIMWA: AIBU WATOTO WETU KUFANYA KAZI ZA NDANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
MBUNGE wa Kalenga mkoani Iringa Godfrey Mgimwa amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwapeleka watoto wao waliohitimu darasa la saba kufanya kazi za ndani mijini kwa kuwa ni aibu kwa wakazi wa mkoa huo.
Akizungumza katika mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi Kalenga na Kiponzelo juzi mbunge Mgimwa alisema kuwa mkoa wa Iringa umekuwa ukisifika kwa kutoa wafanyakazi wa ndani jambo ambalo ni aibu na asingependa jimbo lake kuwa katika orodha ya yanayosifika kwa hilo.
Mbunge huyo, alisema kwa muda ambao atakuwepo madarakani kama mbunge, atafurahi kuona wazazi wanawasomesha watoto wao elimu ya Sekondari ama ufundi ili kuja kuwasaidia mbeleni, badala ya kuwaruhusu kwenda mijini kutumikishwa kazi za ndani na kwenye madanguro, ambako yanaweza kuwasababishia kurudi kijijini na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
"Wazazi wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba katika shule zote za msingi jimbo langu la Kalenga, ninaomba sana kuungana katika kulijenga jimbo kwa kutowaruhusu watu wenye nia mbaya kuja kukusanya watoto wetu na kuwapeleka mijini katika kazi za ndani na madanguro," alisema.
Alisema kitendo cha baadhi ya wazazi kutopenda kuwasomesha watoto elimu ya sekondari na kuwaruhusu kwenda kufanya kazi ya ndani si heshima kwa  Kalenga na mkoa mzima, bali ni aibu kubwa ambayo kama isipo kemewa itajenga dhana ya kuwa Iringa ni kisima cha wafanyakazi wa ndani.
  Mgimwa alisema kuwa umefika wakati kwa wakazi wa Iringa kuungana pamoja na kuugeuza mkoa huo kuwa wa maendeleo badala ya kuwa wa kuzalisha wafanyakazi wa ndani.
Katika mafahali hayo, Mgimwa alijitolea kusaidia ujenzi wa choo cha wanafunzi katika shule ya Msingi Kalenga kwa kutoa fedha za kununua bati  43 pamoja na kusaidia ujenzi wa vyoo vya matundu 18 ya wanafunzi katika shule ya msingi Kiponzelo.
 Chanzo:Tanzania Daima

JUMUIYA YA WATUMIAJI MAJI NZIHI WAPATIWA PIKIPIKI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
MKURUGENZI wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Kampuni ya Simu Tigo, Jackson Kiswaga ametoa msaada wa pikipiki kwa jumuiya ya Watumiaji Maji Kata ya Nzihi kwa lengo la kumaliza kero iliyokuwa inawakabili ya usafiri ili kuwawezesha kutembelea mitambo mbalimbali kwa urahisi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika hivi karibuni katika ofisi za kata hiyo, Kiswaga aliahidi kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuwaletea maendeleo.
Alisema apatapo fursa ya kukutana na watu wa ndani na nje ya nchi wanaoweza kusaidia maendeleo ya watu wengine amekuwa akiyakumbuka matatizo ya wananchi wa Iringa na kuomba msaada.
“Hakika katika kuleta maendeleo nitahakikisha nashirikiana na wenzangu katika maendeleo yetu, sitaacha kutoa mchango wangu, nimefanya hivyo muda mrefu uliopita, nafanya hivi sasa na nitaendelea kwa siku zijazo,  nimekutana na wadau kutoka Marekani, Ulaya na Afrika Kusini kuna mambo yanakuja katika sekta ya afya na elimu na yatakapokuwa tayari nitawaleta ,”  alisema Kiswaga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nzihi, alisema chombo hicho cha usafiri kitaiwezesha jumuiya hiyo kusafiri eneo moja hadi lingine kufuatilia maendeleo na changamoto zinazoukabili mradi huo wa maji.
Naye Meneja wa Watumiaji Maji Kata hiyo, Hamza Chorobi, alisema mradi huo wa maji una changamoto kama vile uchakavu wa miundombinu yake na ongezeko la watumiaji wa huduma hiyo, hivyo unahitaji zaidi ya sh milioni 300 kwa ajili ya ukarabati.
Chanzo:Tanzania Daima

CHADEMA: POLISI WANAANDAMANA BILA KUJUA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
CHADEMA: Polisi wanaandamana bila kujuaCHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Iringa Mjini, jana kimeshindwa kufanya maandamano ya amani kama ilivyotangazwa kwa kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wake, Frank Nyalusi, kuzuiliwa na jeshi la polisi mkoani hapa.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Nyalusi ambaye ni diwani wa Mivinjeni, alisema kuwa maandamano yanayofanyika mkoani hapa licha ya zuio la jeshi la polisi ni ya kisasa zaidi, kwa kuwa yanawahusu askari wenyewe kuandamana kwa kuweka ulinzi, hivyo kuandamana wao pasipo kujua.
Alisema jeshi la polisi linaandamana nchi nzima kwa kuwakea ulinzi pasipo kujua kuwa, hata wananchi wanaandamana kisasa kwa kuwafuata wao kila wanapokwenda kwa lengo la kujua kama wanachama wa CHADEMA na wafuasi wake wanaandamana.
Alisema walitoa taarifa kwa jeshi hilo siku mbili zilizopita wakielezea nia yao ya kufanya maandamano hayo, ikiwa ni kuitikia wito uliotangazwa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe wa kufanya maandamano ya amani yasio na ukomo yenye lengo la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba.
Alisema pamoja na jeshi hilo kuwazuia kufanya maandamano hayo, jana hiyo hiyo waliruhusiwa kufanya mkutano wa hadhara uliofanyika katika mtaa wenye wafanyabiashara ndogondogo (Machinga), maarufu kama Magari Mabovu Kata ya Kitanzini.
Wakati CHADEMA wakidai kudhibitiwa kufanya maandamano hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, alisema jeshi hilo halijapokea barua yoyote kutoka chama hicho inayoonesha wameomba kufanya maandamano hayo.
Akitoa ufafanuzi huo kwa njia ya simu, Mungi alisema; “Nchi hii kama zilivyo nchi nyingine inaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni.”
Alisema watanzania bila kujali wanatoka kundi gani ni lazima wafanye mambo wanayotaka kwa kuzingatia sheria, vinginevyo mkono wa sheria utawafukuzia.
 Chanzo Tanzania Daima

WANAWAKE KITELEWASI VINARA KUJIFUNGULIA MAJUMBANI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
WANAWAKE wa Kijiji cha Kitelewasi Kata ya Rungemba Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, wanaongoza kwa kujifungulia majumbani licha ya elimu kutolewa kuhusu umuhimu wa kujifungulia katika vituo vya afya na zahanati.
Akizungumza na Tanzania Daima, muuguzi wa zahanati ya Rungemba, Suzan Mhngole, alisema pamoja na kujitahidi kutoa elimu kijiji hadi kijiji, bado suala la kujifungulia katika zahanati, vituo vya afya na hospitali kwa wananchi wa Kitelewasi ni changamoto.
Mhongole, alisema asilimia kubwa ya wanawake wanaobeba mimba katika kijiji hicho ni wabishi wa kufuata maelekezo na ushauri wa wataalam pindi wanapofika kliniki, na mwishoni hujifungulia majumbani mwao bila kujali matatizo yanayoweza kujitokeza.
Alitaja sababu za kujifungulia majumbani ni kuwa, wengi wanapopewa rufaa ya kwenda kujifungulia hospitali ya Wilaya, wamekuwa hawafanyi hivyo na badala yake huenda kujifungulia majumbani.
“Tunapogundua kuwa mjamzito ana vidokezo vya hatari, tunamuandikia rufaa ya kwenda katika hospitali kubwa lakini wengi tunaowaandikia rufaa… wamekuwa hawaendi na badala yake wanaamua kwenda kujifungulia majumbani mwao,” alisema.
Kata ya Rungemba ina vijiji vitatu, ambavyo vyenye zahanati ni Rungemba na Itimbo huku Kitelewasi ikiwa haijakamilika kujengwa.
 Chanzo:Tanzania Daima

MAANDAMANO YA CHADEMA IRINGA YAPIGWA STOP, WARUHUSIWA KUFANYA MKUTANO WA HADHARA
Frank Nyalusi, Mwenyekiti wa Chadema Iringa Mjini

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jimbo la Iringa Mjini jana limeshindwa kufanya maandamano ya amani kama ilivyotangazwa kwa kile kilichoelezwa na Mwenyekiti wake, Frank Nyalusi “tumepokea zuio kali kutoka jeshi la Polisi.”Akizungumza na habarileo jana, Nyalusi alisema walitoa taarifa kwa jeshi hilo siku mbili zilizopita wakielezea nia yao ya kufanya maandamano hayo ikiwa ni kuitikia wito uliotangazwa na Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe wa kufanya maandamano ya amani yasio na ukomo yenye lengo la kushinikiza kusitishwa kwa Bunge la Katiba.Alisema pamoja na jeshi hilo kuwazuia kufanya maandamano hayo, jana hiyo hiyo waliruhusiwa kufanya mkutano wa hadhara uliotarajiwa kufanyika mtaa wenye machinga wengi maarufu kama magari mabovu, Kitanzini.“Kwahiyo tutakuwa na mkutano wa hadhara utakaohutubiwa na mimi mwenyewe na viongozi wengine wa chama kuanzia saa 10 jioni, hivisasa tupo kwenye kikao cha kamati tendaji kuweka maazimio kuhusu zuio la maandamano hayo ya amani” alisema kwa njia ya simu.Akieleza kushangazwa na maamuzi ya Polisi ya kuzuia maandamano yao, Nyalusi alisema maazimio yatakayofikiwa katika kikao hicho atayatangaza kwenye mkutano huo.Wakati Chadema wakidai kudhibitiwa kufanya maandamano hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema jeshi hilo halijapokea barua yoyote kutoka katika chama hicho inayoonesha wameomba kufanya maandamano hayo.Akitoa ufafanuzi huo kwa njia ya simu, Mungi alisema “nchi hii kama zilivyo nchi nyingine inaendeshwa kwa sheria, taratibu na kanuni.”Alisema watanzania bila kujali wanatoka kundi gani ni lazima wafanye mambo wanayotaka kufanya kwa kuzingatia sheria vinginevyo mkono wa sheria utawafukuzia.Alisema mji wa Iringa upo shwari na kwamba jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kukabiliana na hali yoyote ile itakayoonekana inataka kuhatarisha amani.Aliwataka wakazi wa Iringa kuendelea na shughuli zao kama kawaida na pale watakahisi au kusikia kuna mtu au kikundi chochote cha watu kinataka kufanya jambo linaloweza kuhatarisha usalama wao na wa mali zao, watoe ushirikiano 

kwa kutoa taarifa Polisi. Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

IRINGA WAONYWA ‘VISHOKA’ WA MAJI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
MAMLAKA ya majisafi na majitaka Manispaa ya Iringa (Iruwasa), imewaasa wananchi kuwa makini na uunganishaji maji kinyemela kwenye mtandao wa huduma hiyo kuepuka usumbufu na sheria kali zitakazochukuliwa dhidi ya watakaobainika.
Msimamizi Mkuu Kitengo cha majitaka na usafi wa mazingira Iruwasa, Yohana Bugando, alisema kumekuwa na ongezeko la wananchi wanaounganishiwa huduma ya majisafi na taka kwa kutumia mabomba ‘feki’ na mafundi ambao hujitambulisha wametumwa na mamlaka hiyo kumbe ni ‘vishoka’.
Bugando, aliongeza kuwa hali hiyo husababisha kupotea kwa maji kutokana na mabomba kupasuka na kuvuja mitaani kutokana na kutokuwa imara.
Aliwaasa wananchi kufuata utaratibu wa kuunganishiwa huduma ya maji kwa kutuma maombi kwa uongozi wa serikali za mitaa, maofisa ardhi wa eneo husika na hatimaye Iruwasa ndiyo yenye mamlaka ya kutoa huduma ya uunganishaji wa mtandao wa maji safi na taka.
Aliongeza kuwa, Iruwasa inaendelea na mpango wa kuhakikisha wakazi wa Kata za Ilala, Makorongoni, Mivinjeni na Gangilonga Manispaa ya Iringa, wanaunganishwa na huduma ya maji taka hivyo wananchi waepuke kutupa vitu vigumu na mchanga kwenye mabomba ya maji taka.
 Chanzo:Tanzani Daima

MJENGWABLOG IMETIMIZA MIAKA MINANE NA TUNASONGA MBELE!


Ndugu zangu,
LEO ni Septemba 19, ni Siku ya Kuzaliwa Mtandao wa Mjengwablog.
Kwa mwanadamu, hakupaswi kuwapo na ukomo wa kujitahidi kufanya yalo mema kwa jamii yako.
Na katika kujitahidi kuyafanya yalo mema, basi, mwanadamu uwe tayari kukumbana na changamoto nyingi. Na kama ilivyo kwa maji ya mto, yanapokutana na mwamba, basi, kasi yake huongezeka maradufu.
Leo blogu yako hii ya Mjengwablog imetimiza miaka minane. Miaka minane si haba. Kwa mtoto, aweza kuwa darasa la Pili. Na kwetu wa Mjengwablog ni miaka minane ya kujifunza, kukosea, kujifunza kutokana na makosa, na kisha kusonga mbele.
Kwa niaba ya timu nzima ya Mjengwablog nachukua fursa hii kuwashukuru, kwanza kabisa, mke wangu mpenzi, Mia, ambaye, bila yeye, kazi hii yangu ya kuitumikia jamii ingelikuwa ngumu sana. Pili, niwashukuru kwa dhati wanangu wanne, Olle, John, Manfred na Gustav. Wanawangu hawa wamekuwa na mchango mkubwa pia, ikiwamo kufanya utani na mimi baba yao, ilimradi niwe na wakati wa kucheka, hata pale nilipoona kazi ni ngumu na kukutana na vikwazo.
Na kwa dhati kabisa, naishukuru timu nzima ya Mjengwablog. Nawashukuru kwa upekee kabisa Wanafamilia wote wa Mjengwablog, ukiwamo wewe unayesoma maandiko haya sasa, maana, bila nyinyi, kusingekuwa na maana ya kuifanya kazi hii. Mmekuwa nasi katika hali zote. Hivyo basi, kutuunga mkono.
Naam, ni miaka minane ya kuwa mtandaoni karibu katika kila siku inayotujia na kupita. Ni miaka minane ya mapambano magumu ya kuitumikia jamii na kuhakikisha kuwa tunabaki hai.
Maana, unapoamua kuitumikia jamii bila kuegemea upande, basi, ina maana pia ya kujiweka katika mazingira ya hatari sana. Yumkini kuna maua mengi ya upendo yanaweza kurushwa kwako, lakini, kuna mishale michache ya sumu ambayo pia itarushwa kwako. Kwamba kuna maadui pia.
Na ukimwona nyani ametimiza miaka minane , basi, ujue kuna mishale kadhaa ameikwepa. Lakini, na anavyozidi kuendelea kuishi, yumkini kuna mishale mingine inaandaliwa. Na nyani hatakiwi kuishi kwa kuogopa mishale ya wanadamu. Vinginevyo, ajitundike mtini, afe.
Lililo jema na kutia faraja ni kutambua, kuwa kuna walio wengi wenye kufaidika na kazi hii ya kijamii ambayo Mjengwablog inaifanya. Ni hawa ndio wenye kututia nguvu ya kuendelea kuifanya kazi hii pamoja na changamoto zake nyingi.
Ndugu zangu,
Ilikuwa ni Jumanne, Septemba 19, 2006. Ni siku hiyo ndipo kwa mara ya kwanza niliingiza picha ya kwanza kwenye mjengwablog na kuashiria uzinduzi wa blogu. Ni picha hiyo inayoonekana hapo juu. Niliipiga eneo la Kinondoni Shamba. Tangu siku ya kwanza, niliweka wazi kwenye fikra zangu, kuwa Mjengwablog iwe jukwaa litakalomtanguliza mtu wa kawaida. Iwe sauti ya wale ambao sauti zao hazisikiki.
Na Mjengwablog ikawa chachu ya kuanzishwa kwa gazeti la michezo na burudani la ’ Gozi Spoti’, ikawa chachu pia ya kuanzishwa gazeti la ’ Kwanza Jamii’.
Na kuna miongoni mwetu wenye kufikiri, kuwa mwenye kumiliki gazeti ni lazima awe Mhindi au Mtanzania ’ mweusi’ Mfanyabiashara tajiri. Nakumbuka kuna hata ambao hawakuwa tayari kuchangia kiuandishi kwenye ’ Gozi Spoti’ na ’ Kwanza Jamii’ kwa vile linamilikiwa na ’ Mswahili mwenzao!’Na hata kupata matangazo kukawa na ugumu mkubwa. Gozi Spoti lilisimama kuchapwa baada ya mwaka mmoja mitaani. Kwanza Jamii, nalo likasimama kuchapwa. Likarudi tena baada ya kuingia ubia na Shirika la Daraja. Baada ya miaka miwili na baada ya aliyepelekea kuingia ubia kuondoka nchini na kurudi kwao Uingereza, basi, Kwanza Jamii nalo ’ likaandaliwa’ mazingira ya kuondoka mitaani.
Hata hivyo, Kwanza Jamii, gazeti dogo, ambalo naamini ni muhimu kwa jamii, limerudi tena kwa kutolewa bure kanda ya Nyanda za Juu Kusini na kwa kupitia mtandaoni. Mipango iko mbioni kuliimarisha zaidi katika siku zijazo.
Ndugu zangu,
Changamoto zipo ili tukabiliane nazo, na si kukata tamaa. Mjengwablog inatimiza miaka minane leo kwa vile tulishaamua, kuwa tutapambana hadi risasi ya mwisho. Hivyo pia, tutapambana hadi pumzi ya mwisho.

Maana, tunaamini kuwa kazi tuifanyayo ni yenye manufaa kwa jamii pana. Na tuna haki ya kuifanya. Tunavumilia sauti zenye kutushutumu na kutukosoa. Kuna tunayojifunza kutoka kwa wakosoaji wetu. Tunawashukuru sana na tunawaomba waendelee kutukosoa kila wanapoziona kasoro.
Chini hapa ni maoni ya kwanza kabisa kutumwa na mtembeleaji. Na anachoandika mtembeleaji huyu kutoka India kinaakisi dhamira niliyokuwa nayo.
Bwana huyu anasema; { fakir005 } at: Tue Sep 19, 06:32:00 PM EAT said... This looks like an African blog. Once the TV showed an African milk his cow. The cow had so stretched tits. I've never seen so much stretching. The african as really stretching further to twice the original length to get any drop of milk he could get. It was obvious the cow was dry because it was too long after the birth of her calf and needed to be inseminated again.The cow just stood there while the African worked the Tits. The picture does not show anycows. But the man in the picture and the house remind me of the TV scene in the gone years."

Maggid,
Mwenyekiti Mtendaji.
Mjengwablog.com


Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa