Home » » Naiona Afrika Ikiinuka Tena Kiuchumi.

Naiona Afrika Ikiinuka Tena Kiuchumi.



Na: Albert Sanga- Iringa.

Mwaka 2001 nilihudhuria kongamano la kidini ambalo pamoja na mambo mengine lilijadili hali ya maendeleo ya Afrika. Kongamano hilo lilifanyika katika shule ya sekondari ya Bihawana iliyopo nje kidogo ya mji wa Dodoma. Mada iliyowasilishwa kuhusu Afrika ilikua na kichwa, “Je, Afrika imelaaniwa?”. 

Mtoa mada mkuu alikua ni mzungu mmoja (mmishenari), ambaye aliamsha mjadala mkali kweli kweli mara baada ya kumaliza kuwasilisha hoja zake. Katika mjadala uliofuatia (baada ya mtoa hoja kumaliza) kulijitokeza makundi mawili baina ya wanakongamano; moja likisema na kuamini kua Afrika imelaaniwa na jingine likipinga kabisa laana ya Afrika. Upande uliokua ukisema Afrika imelaaniwa ulikua na hoja zenye nguvu kweli kweli na ulionekana kuuzidi ule upande uliopinga laana ya Afrika.



Mmoja wa wachangiaji alisimama na kusema maneno yafuatayo, “Ndugu zangu mimi nawathibitishia kua Afrika tumelaaniwa na uthibitisho huu tunaupata kutoka kwenye Biblia katika Kumbukumbu la Torati 28: 15- 40. Biblia inasema kuwa; …..utalaaniwa mjini na vijijini, wageni waliopo kati yako watafanikiwa wewe ukididimia, utapanda mzabibu nawe hutakula matunda yake, utaandamwa na vita na magonjwa, utadhulumiwa rasilimali zako…..; Kwa maandiko haya mnabisha nini kusema Afrika imelaaniwa?”.



Mchangiaji mwingine ninaemkumbuka ambae aliamsha hisia tafakarishi miongoni mwa wote tuliokuwepo pale alieleza mwonekano wa kijiografia wa Afrika akiulinganisha na laana. Yeye alisema hivi, “Afrika imelaaniwa na uthibitisho tunaweza kuupata hata kutoka kwenye ramani ya Afrika yenyewe. Ramani ya Afrika ina umbo la kiulizo hii ina maana kua tutakua watu wa kuandamwa na mambo yasiyo na majibu maisha yetu yote”.



Upande uliokua ukipinga ulifurukuta kweli kweli ukitumia hoja ambazo japo kuwa zilionekana kua na mantiki lakini zilikosa nguvu na ushawishi wa kutosha. Mathalani upande huu ulisema, Afrika haijalaaniwa kwa sababu Yesu Kristo alipozaliwa baba na mama yake waliambiwa na malaika wakimbile Afrika katika nchi ya Misri.  Kwa maana hii Afrika ilimlea mkombozi wa ulimwengu.



Hadi leo hoja zilizokua zikisema Afrika imelaaniwa zingali zimenasa katika akili yangu kutokana na namna zilivyokua zinagusa picha halisi ya Afrika. Baada ya mjadala huo mtoa mada alisimama na kuhitimisha mjadala kwa kusema maneno yafuatayo, “Inawezekana Afrika ikawa imelaaniwa na inawezekana ikawa haijalaaniwa. Hayo yote sio mambo ya kujishughulisha nayo; ila tunatakiwa kujishughulisha na ukweli uliopo ya kwamba watu wote ni mali ya Mungu. Mungu huyu anasema kua anawawazia mambo mema watu wake, wakiwamo watu wa Afrika. “



“Hakuna sababu ya kukata tamaa ya maisha eti kwa sababu Afrika imelaaniwa, kwa sababu unaweza kuishi maisha kama ya Ulaya hata ukiwa Afrika na msisahau kuwa hata katika nchi zilizoendelea kuna masikini wa kutupwa ambao wanaitamani sana Afrika.”. Baada ya kuhitimisha huko wahudhuriaji wote tuliingia kwenye maombi ya siku mbili kuiombea Afrika ipokee ‘upya’ na rehema za Mungu.



Imepita miaka takribani kumi tangu nishiriki kwenye mjadala na hatimaye maombi kuhusu Afrika. Katika miaka hii kumi nimeshuhudia mabadiliko makubwa yakitokea katika maendeleo ya Afrika kiasi ambacho najiridhisha kua maombi ya watu kwa Mungu kuhusu Afrika bila shaka yamesikika na Mungu ameamua ashuke ‘upya’ hapa Afrika



Kuna msemo maarufu sana usemao, ‘historia hujirudia’ na hilo naona limeanza kutimia kwa Afrika. Wafuatiliaji wa historia bila shaka wanakumbuka kuwa Afrika ilitangulia kupata maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii kabla hata ya Ulaya. Bara hili lilikua na viwanda, lilikua na dola kubwa na zenye nguvu sana tena zilizoendeshwa kidemokrasia na kwa utulivu mkubwa. Gunduzi nyingi za kisayansi, lugha na kijamii zilitokea Afrika ikiwemo ugunduzi wa umeme, maandishi ya kwanza, kalenda na hata uhandisi wa majengo.



Vyuo vikuu vya kale kabisa duniani vinapatikana Afrika hii ikitupa picha moja kuwa hata kielimu Afrika ilianza na wengine wakafuata. Orodha ya maendeleo ya Afrika yaliyokuwepo kabla ya kuingia kwa ukoloni ni ndefu sana lakini itoshe tu kusema ujio wa ukoloni uliivuruga ‘kabisa’ Afrika. Lakini ile historia ya maendeleo iliyovurugwa na wakoloni sasa imeanza kujitokeza kwa upya tena. Afrika imeanza kuinuka.



Yanayoendelea Afrika kwa sasa yanatia moyo sana kiasi kwamba hata ile misemo ya kifedhuli kwamba, “Afrika ni bara la giza”, “Afrika ni kisima cha vita na migogoro” inazidi kupoteza mashiko kwa kasi ya ajabu. Bila shaka hata viranja wa magharibi ambao wanaimba kuhusu demokrasia nao wanashangaa yanayotokea Afrika. Ile demokrasia yetu ya ustaarabu na uungwana sasa inatumika. Vyama vya siasa vinabadilishana madaraka kwa amani, udikteta unazidi kutokomea, ukibaraka wa viongozi wa Afrika kwa ‘wamagharibi’ unayoyoma kwa kasi ya ajabu.



Siku zote masikini hafilisiki na anaeinuliwa ni yule aliyechini. Kama tukiwa makini kutafsiri hali tete za kichumi zinazoendelea duniani tunaweza kuelewa bila shida mambo yafuatayo; Afrika kwa sababu ni masikini haina kitu kikubwa cha kupoteza lakini kwa sababu ipo chini ina nafasi ya kuinuliwa.



Anaefilisika ni tajiri, mwenye kitu ndio hupoteza na aliye juu ndie hushuka. Nchi za magharibi zinaporomoka kwa kasi na sasa zinapeana mbeleko kuzuiana zisifilisike, lakini wapi! Zinaendelea kupoteza rasilimali, zinapoteza ushawishi na zinahaha na kutoa jasho. Walisema waswahili adui yako mwombee njaa; hii ni saa ya Afrika kuinuka tena!



Ripoti za kimataifa pamoja na hali mbalimbali tunazozishuhudia zinaeleza picha kamili ya namna hatua za Afrika zinavyoongezeka hata kama ni pole pole. Kumekua na ripoti za tafiti mbalimbali kuihusu Afrika zinazotolewa na vyanzo tofauti tofauti yakiwemo mashirika makubwa ya kimataifa , nchi za magharibi na mawakala wao. Baadhi ya watoa maoni wanasema ripoti hizi zimekua zikichora picha hasi kuhusu hali na maendeleo ya Afrika. Na mahali ambapo zinachora picha chanya basi unakuta eidha ni kwa maslahi fulani ama ni kutaka kuonesha kuwa walitoa msaada ambao umeleta tija.



Kwa maana hii tunapoitazama Afrika inayoinuka tena ni busara sana kutumia vyanzo huru vya takwimu na uhalisi wa mambo katika tathmini zetu wenyewe. Hata hivyo ripoti na takwimu zinazolalamikiwa kuikandamiza Afrika zingali zinatufaa kwa kua iwe kwa wema ama kwa ubaya zingali  zinabeba kitu fulani kuhusu Afrika



Kwa upande wa uchumi (eneo ambalo tumekua hatujiwezi kwa miaka mingi) hali inatia moyo sana. Katika nchi kumi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi sana duniani nchi sita zinatoka katika bara la Afrika; zikiongozwa na Ghana ambayo uchumi wake unakua kwa kasi ya asilimia 13%. Ghana ndio nchi inayoongoza kwa kua taifa lenye uchumi unaokua kwa kasi kuliko mataifa yote duniani.



Ghana yetu imezitupa mbali kabisa hata nchi nyingi za Ulaya ambazo uchumi wake unajikongoja kukua kwa asilimia moja. Mataifa ya Afrika ambayo uchumi wake unakua kwa kasi yameshayapiku hata yale mataifa ya Asia ambayo yanafahamika kama “Asian Tigers”. Mwaka huu pekee, uchumi wa bara la Afrika unakadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia 6%, hii ni hatua kubwa kutoka mgando wa uchumi katika asilimia 4% kwa miaka ya nyuma.



Nimesema hapo juu ya kwamba adui yako mwombee njaa ndipo utamshinda kirahisi. Hadi sasa kuna mataifa ya Ulaya ambayo yanahenyeshwa na mzigo wa madeni kuliko mataifa ya Afrika. Leo hii nchi ya Angola kutoka Afrika inaikopesha fedha na kuipa misaada nchi ya Ureno. Kumbuka kuwa Ureno iliitawala Angola wakati wa ukoloni lakini leo Ureno imegeuka kuilamba miguu Angola-huu ni muujiza!



Benki yetu ya nyumbani, ‘African Development Bank-AfDB’ kupitia ripoti yake ya kiuchumi inasema kua ifikapo mwaka 2060 watu wa uchumi wa kada ya kati watakua ni asilimia 42 ikiwa ni ongezeko la asilimia 10 ukilinganisha na idadi iliyopo kwa sasa. Miaka 50 ijayo inatazamiwa kuwa idadi ya watu watakaokuwa wakiishi chini ya mstari wa umasikini uliopindukia watakua ni chini ya asilimia 30. Hii ina maana kua umasikini unaendelea kupungua kwa kasi ya ajabu na uchumi unazidi kupaa ukilinganisha na hapo zamani.



Kukua huko kwa uchumi kunaleta mwanga wa kuongezeka kwa biashara na uwekezaji. Ushahidi tunaweza kuupata kwa kuyaangalia makampuni ya kibiashara ya Afrika namna yanavyoshindana na kutunisha misuli katika anga za kimataifa. Mathalani, kampuni ya South Africa Breweries Miller (SAB) ya nchini Afrika kusini hivi karibuni iliinunua kampuni ya American Breweries ya nchini Marekani.



Hii inaifanya SAB kuwa kampuni ya pili kwa ukubwa duniani miongoni mwa makampuni ya vinywaji vya pombe. Jambo kama hili usongelitazamia kutokea katika miaka ya ‘giza’ la Afrika. Huu ni mfano mmoja kati ya mifano lukuki ambapo kwa sasa ni kawaida makampuni makubwa ya magharibi kuyapigia magoto makampuni ya Kiafrika yakiomba eidha kuokolewa kifedha ama kununuliwa.



Miaka ya zamani kuna hadithi tulikua tunazipata eti kule Ulaya kuna watu ambao hata hawajui hiyo Afrika iko upande gani duniani! Inadaiwa walijifanya ‘kuipotezea’ kwa sababu Afrika ilikua haijisomi kwa kila kitu. Lakini sasa ni tofauti kwa sababu hata makampuni yale makubwa na yenye viburi yanakimbizana kuja kuwekeza na kuuza Afrika. Jirani zetu nchi ya Kenya kuna mamia ya makampuni ya teknolojia kiasi cha kwamba Nairobi imebatizwa kama kitovu cha teknolojia ya mawasiliano kusini mwa jangwa la Sahara.



Sisi waafrika wenyewe wala hatuhitaji takwimu za ‘kumulika na tochi’ kujua kua huu ni wakati wetu bali tunajionea mabadiliko. Wana na binti zetu waliokimbilia ughaibuni kwa ajili ya kusaka maisha mazuri kwa sasa wanarejea kwa kasi kwa sababu wameshajua kua huku nyumbani kuna neema. Mafanikio waliyoyafuata Ulaya kwa sasa yanapatikana katika nchi zao walizozikimbia.



Ingawa kungali na changamoto lakini naiona Afrika ikiinuka tena!





0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa