Home » » CWT yaomba JPM azungumze jambo kuhusu madai yao

CWT yaomba JPM azungumze jambo kuhusu madai yao

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Iringa kimempigia magoti Rais John Magufuli kikimuomba azungumze lolote kuhusu madai ya walimu wakati wakijiandaa kuingia mwaka mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Iringa, Stanslaus Mhongole alisema katika kipindi ambacho baadhi ya watanzania wanalalamikia ukata, kwa upande wao ni kama madai yao ya msingi yamesimama kushughulikiwa.
“Tunamuomba Rais awape walimu furaha, aondoe ukimya juu yetu, natamani kabla mwaka haujaisha aseme chochote kuhusu madai yetu maana tumepiga kelele kwa miaka mingi,” alisema Mhongole.
Mbali na madeni aliyosema yanaendelea kushughulikiwa na serikali, Mhongole aliyataja madai yao mengine ya msingi kuwa ni pamoja na posho ya kufundishia na upandaji wa madaraja.
Alisema posho ni kilio chao cha muda mrefu, upandaji wa madaraja ni jambo linalomuondoa mwalimu kutoka katika ngazi moja ya mshahara kwenda ngazi nyingine.
Alisema kwa miaka mingi walimu wamekuwa wanyonge katika Taifa na akamuomba Rais Magufuli ambaye ni kiongozi aliyedhamiria kuwasaidia wanyonge wan chi hii, kutupia jicho la haraka kwa walimu.
“Kama madaktari, wanajeshi na watumishi wengine wanapata posho, kwanini walimu ambao kazi yao kubwa ni kutengeneza akili za watu wakiwemo viongozi na watalaamu wa nchi hii, hawatazamwi ipasavyo?” alihoji.
Aliipongeza serikali ya Magufuli kwa kuanza kutoa posho kwa wakuu wa shule na waratibu wa elimu lakini akasema walimu washika kazi wanapaswa kutazamwa kwa jicho hilo hilo kutokana na ugumu na unyeti wa kazi yao.
“Na niipongeze pia serikali yake kwa kuandika historia nyingine katika maendeleo ya sekta hiyo. Kwa mara ya kwanza mwaka huu, walimu waliosimamia mitihadi ya darasa la nne walipata posho, haijawahi kutokea,” alisema.
Pamoja na jitihada hizo, Mhongole aliuliza ni lini Magufuli atakutana na CWT ili waweze kumueleza changamoto zao kwa kina.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa