Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Soko kuu Manispaa ya Iringa.
Unapozungumzia soko ni kitu muhimu sana, kwani mji wowote ukikosa soko, unaelezwa haujakamilika.
Hiyo ndiyo hali iliyoko katika Manispaa ya Iringa, ambako kuna masoko kadhaa.
Mwenyekiti wa Masoko ya Manispaa ya Iringa, Sturmi Fussy, anasema
hali ya masoko kwa Manispaa ya Iringa ni nzuri kibiashara, kulinganisha
na mwaka jana, kwa sababu vitu mbalimbali vinapatikana ndani ya sokoni.
Fussy ambaye ni mfanyabiashara wa bidhaa mbalimbali zikiwamo za
ndani (dukani) na vyakula kama vie mchele, anasema mzunguko wa fedha ni
wa wastani.
Anasema, biashara kwa jumla ipo kwa wastani unaowezesha kuendesha maisha ya wana - Iringa.
“Tunaweza kusema mzunguko wa fedha ni mzuri, kwa sababu kama bidhaa
zinapatikana na zinanunuliwa kwa haraka mzunguko unakuwa safi, lakini
kama bidhaa hazipatikani mzunguko nao unakuwa sio mkubwa,” Fussy anatoa
tafsiri ya kibiashara.
Anasema wao wafanyabiashara walipendekeza vituo vya mabasi viwe
karibu na masoko ili wasafiri wanaoingia na kutoka, waweze kununua
bidhaa kwenye masoko hayo, lakini vituo hivyo vimekuwa mbali na eneo la
soko.
Fussy anaongeza kuwa, Soko Kuu la Iringa limezungukwa na vituo vya
kutolea huduma za kijamii kama vile Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Iringa, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Magereza, Kituo
cha Kikuu cha Polisi Iringa na kadhalika.
Anasema, iwapo kituo cha mabasi kingekuwa karibu na soko, watu wote
wangenunua bidhaa sokoni, kwani wapo wanaonunua kwa ajili ya matumizi
ya nyumbani na wengine kwa ajili ya kuuza.
Fussy anasema kuwa, hali ya biashara kwa mwaka jana na mwaka huu
imekuwa tofauti, kwa sababu mwaka jana ulikuwa na ukame, tofauti na
mwaka huu.
“Mfano mwaka jana mchele ulikuwa kwa kilo moja ulikuwa Sh 2400,
lakini kwa mwaka huu kilo moja Sh.1900, ndio maana nikasema bora mwaka
huu kuna neema kidogo kuliko mwaka jana. Hata hivyo, mvua zinaendelea
kunyesha, naamini hata wakulima watalima mazao na chakula kitapatikana
cha kutosha” anasema Fussy.
Anafafanua kuwa Manispaa ya Iringa ina masoko saba, ambayo ni Soko
Kuu, Soko Dogo la Mshindo, Mashine Tatu, Mlandege, Magari Mabavu,
Ipogolo na Kihesa.
Fussy anafanya ulinganishi akisema kuwa Soko la Mashine Tatu lina
biashara nzuri kutokana na kuwa katika eneo lenye mzunguko mkubwa wa
fedha.
Anafafanua kuwa, sababu kuu ni kwamba abiria wa mjini wanashukia
Stendi Kuu ya Mabasi yaendeyo mikoani na kutumia fursa ya kununua vitu
ndani ya soko hilo, pia lipo karibu na stendi.
HISTORIA YA SOKO
Mkuu wa Soko Kuu la Iringa, Michael Mage anasema historia yake ina
mizizi mirefu katika zama zilizopita, Soko C, ambalo lilijengwa mwaka
1896, katika zama za utawala wa Kijerumani, likiwa na vizimba vichache
kwa wakati huo.
Mage anasema kuwa hali hiyo iliendelea hadi mwaka 1972 ikiwa ni
miaka 11 ya taifa kupata uhuru toka kwenye koloni la Waingereza,
walipata sehemu ya kuongeza soko hilo, kukidhi mahitaji ya ongezeko
kubwa la watu.
“Sehemu tulipopata soko jingine, awali ilikuwa stendi. Tukaamua
kuwahamisha na kuweka soko jingine, ili kuweza kukidhi mahitaji ya watu
na tulifanya hivyo kutokana na ongezeko la watu,” anasema Michael .
Anasema sehemu iliyokuwa stendi, walijenga vizimba 176, baada ya
kukabiliwa na ongezeko la watu mwaka 1972. Pia, mwaka 2009 ilifanyika
ongezeko la vizimba.
Mage anasema kuwa, waliongeza wafanyabiashara 147 na ndio sababu ya kuonekana vioski nje ya soko na vizimba vipya ndani ya soko.
Mkuu huyo wa soko anasema kuwa, nafasi katika soko hilo imejaa na
kinachofanyika ni kutangaza nafasi katika soko la Kihesa,
Kitwiru,Ipogolo, Kitanzini, Mlandege.
CHANGAMOTO
Anasema changamoto wanayokumbana nayo ni pale anapowaambia
wafanyabiashara kwenda kwenye masoko mengine, huwa wanagoma na kusema
Soko Kuu ndio ‘Senta’ ya biashara na hivyo kufanya biashara zao kando ya
soko au barabara.
Mage anasema changamoto nyingine, ni kwamba wafanyabiashara
wanaendesha shughuli zao katika sehemu zisizo rasmi na ndicho
kinachowafanya wenye vizimba kutouza bidhaa zao sana.
“Tutawafukuza leo, lakini kesho utakuta wamerudi. Ila sehemu za
kuwahamishia tunazo na wao hawataki kwenda kwenye masoko hayo,” anasema
Michael.
Aidha, anasema biashara kwa kipindi cha mvua ni ngumu, kutokana na biashara ya mali mbichi kuoza kutokana na kunyeshewa.
“Unaweza kuagiza mzigo wa matunda gari zima lakini mzigo huo
unaishia jalalani kutokana na kuharibika. Mfano, matunda hayo yanaishia
jalalani na unakuta mtu kaleta mzigo kabla ya kuingiza mezani, tayari
asilimia kubwa umeshaharibika,” anasema
Mage anasema, kwa sasa wamejipanga kuboresha masoko yao ili yawe ya
kisasa hasa kwa masoko ya Kihesa na Mlandege, ili yakidhi mahitaji ya
wafanyabiashara wake.
KAULI YA WAFANYABIASHARA
Rajab Mtatifikolo, anayeuza viazi mviringo mjini Iringa, anasema
mwezi Januari biashara haikuwa nzuri, kwa sababu sehemu kubwa ya bajeti
ya wateja ilielekezwa kwenye mahitaji ya watoto wao.
Anasema, changamoto waliyokumbana nayo katika kipindi cha nyuma,
kunyanyaswa na askari mgambo wa Manispaa, hata kunyang’anywa na bidhaa
zao za viazi kwa maana wao wamekuwa wakizunguka zunguka.
“Manispaa wanataka tuuze nje ya mji na nje ya mji ambako hakuna
wanunuzi,wanunuzi wapo katikati ya mji, ndio maana wamekuwa
wakituzungusha na sisi tunategemea bidhaa hii ya kutembeza viazi
mviringo,” anasema Mtatifikolo.
Anasema bei za viazi zinatofautiana, kwani kuna viazi vinavyotoka
mkoa wa Njombe, Mbeya na vingine ni vya Iringa na tofauti kuu inatokana
na gharama za usafirishaji.
Mtafitikolo anataja bei zake kuwa, viazi vinavyotoka Mbeya gunia
moja linauzwa Sh.70, 000; Njombe Sh.80, 000 na Iringa Sh. 65,000.
Anaeleza mtazamo wake kuwa, biashara itakuwa nzuri pale kipindi cha
ununuzi wa vifaa vya wanafunzi kitapita na Mgambo wa Manispaa wataacha
kuwanyanyasa, huku akisisitiza kuwa eneo la katikati ya mji ni muhimu
kwao, kwani lina mzunguko mkubwa wa fedha.
Bligitha Sulemani, anayeuza mchele katika soko la Mashine Tatu,
anasema bei ya mchele inatofautiana kulingana ubora wake na nji kawaida
katika kipindi cha ukame bei ya mchele kupanda.
Anatoa mfano kuwa, mchele unaotoka mkoani Mbeya unapaswa kuuzwa
kwenye Super Market, kwa sababu mauzo yake ni taratibu kutokan ana kuwa
na bei kubwa.
Anaongeza kuwa, mchele unaotoka Iringa eneo la Pawaga, Idodi na
Madibila ambao upo mpakani na Mbeya, bei zake ziko tofauti kuanzia
Sh.1900 hadi Sh. 2400.
“Kwa sasa mchele hauwezi kushuka be, kwa sababu bado wakulima
hawajavuna mpunga mashambani na watakapovuna mwezi wa sita, yawezekana
ukashuka kwa maana kila eneo wanaingiza mchele mpya,” anasema Bligitha
WANUNUZI NA WAUZAJI SOKO KUU
Wateja wa nyanya katika Soko Kuu la Iringa, wanalalamika kuwa
wafanyabiashara wanawauzia nyanya kwa bei ghali kikiwa na kiwango cha
chini, jambo linalofanya washindwe kununua bidhaa hizo.
Stella Aretasi ni mnunuzi anayeeleza kwa mfano kuwa, nyanya inauzwa
kwa kibaba cha maji cha lita moja kwa bei ya Sh.1, 000 mtu akitaka
kiwango cha chini cha nyanya ni Sh. 300 hawezi kupata kwa sababu wanauza
kuanzia Sh.1000 na kuendelea.
Anaongeza kuwa inatakiwa wafanyabishara hao waweke bei ya chini
hata kama mtu wa kiwango cha chini akitaka kununua nyanya moja ya Sh. 50
au Sh. 100 apate, lakini wakiuza kwa kibaba cha lita moja Sh. 1000
wanawaumiza watu wa kiwango cha chini.
Mfanyabiashara anayejitambulisha kwa jina la Baba Sharon, anayeuza
samaki katika Soko kuu la Iringa, anasema bidhaa hiyo sasa haipatikani
kirahisi, sababu ni kukosekana maji katika Bwawa la Mtera.
“Tumekosa samaki wakubwa, kwa sababu ya bwawa kukosa maji. Lakini
tunawaomba watu wanaohusika na bwawa hilo wahakikishe kipindi hiki cha
mvua, wanalijaza bwawa hilo maji ya kutosha ili samaki waendelee
kuzaliana na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu ambao wanaenda
kukinga maji au kufungulia maji kwenye mashamba yao kwa ajili ya
shughuli za kilimo,” anasema na kuongeza:
“Watu wa kiwango cha chini wakiona samaki wadogo kama hawa
wanawakimbilia kwa sababu tunauza bei ya chini, lakini sisi kama
wafanyabishara hatupendi kuuza samaki wadogo ila inatubidi tu.”
Anahiyimisha kuwa, endapo maji yatakuwa yanapatikana ana imani kuwa
samaki watazaliana kwa wingi na watakuwa na samaki wakubwa nao
watapatikana, kuridhisha matakwa ya wateja wote
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment