Home » » PSPF YASAIDIA MABATI IRINGA

PSPF YASAIDIA MABATI IRINGA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

KATIKA kutekeleza maagizo ya Rais Jakaya Kikwete, kila shule iwe na maabara tatu ifikapo Novemba mwaka huu, Mfuko wa Pensheni ya Watumishi wa Umma (PSPSF), umetoa msaada wa mabati 300 yenye thamani ya zaidi ya sh milioni 6 kwa Wilaya za Kilolo na Mufindi mkoani Iringa kufanikisha ujenzi huo na hosteli kwa Chuo cha Ualimu Mufindi.
Wakati Kilolo imepata mabati 200 yatakayotumika kusaidia kukamilisha ujenzi wa maabara unaoendelea katika shule zake za Sekondari, Chuo cha Ualimu Mufundi (MUTCO), cha mjini Mafinga wilayani Mufindi kimepata mabati 100 ikiwa ni kutimiza ahadi iliyotolewa na Meneja wa Sheria wa PSPF, Abrahamu Siyovelwa, aliyoitoa Mei 27 katika mahafali ya chuo hicho.
Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Monica Kalalu, katika viwanja vya MUTCO juzi, Ofisa Mfawidhi wa PSPF Mkoa wa Iringa, Baraka Jumanne, alisema lengo la msaada huo ni sehemu ya mpango wao katika kusaidia sekta ya elimu nchini na kutekeleza maombi yaliyoombwa na viongozi wa wilaya hizo katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais Kikwete kila Sekondari iwe na maabara ifikapo Novemba mwaka huu.
"PSPF ni shirika la mfuko wa pensheni, hivyo faida lazima iifikie jamii hasa katika suala la elimu ya Sekondari na Msingi, hivyo tumeamua kuwapatia mabati 100 chuo cha Ualimu Mufindi na Wilaya ya Kilolo mabati 200 kutekeleza maombi yao kwa shirika la PSPF kusaidia ujenzi wa maabara na ujenzi wa hosteli kwa chuo cha MUTCO, hivyo leo tunawakabidhi mabati haya 300,000 kwa lengo la kutekeleza ahadi ya shirika,” alisema Jumanne.
Akieleza faida ya kujiunga na PSPF, ni kwamba kuna mafao yanayotolewa na mfuko huo yanalenga kuwawezesha watumishi kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utumishi wao kabla na baada ya kustaafu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Kalalu, aliishukuru PSPF kwa msaada huo na kutoa wito kwa wadau wengine wajitokeze kuisaidia sekta ya elimu hususani ujenzi wa maabara ambao unaendelea nchi nzima kwa sasa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Guninita, alisema msaada huo utazisaidia shule za Sekondari katika kukamilisha ujenzi wa maabara na kuwataka PSPF wasiishie hapo katika kutoa msaada zaidi katika sekta ya elimu.
Mwakilishi wa PSPF makao makuu, Amelia Rweyemamu, akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, alisema kuwa PSPF inatambua umuhimu wa kuwepo kwa maabara hapa nchini, hivyo ofisi yake imeona vema kushiri katika ujenzi huo kwa kutoa mabati hayo.
Rweyemamu, alisema PSPF inatoa mafao mbalimbali ikiwa ni pamoja na fao la uzeeni, ulemavu, kifo, mazishi, fao la wategemezi lisilo na kikomo, fao la kujitoa, fao la kufukuzwa kazi na fao la ujasiriamali.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa