Home » » TUME YA UCHAGUZI:CHOPA ZA CHADEMA RUKSA KALENGA

TUME YA UCHAGUZI:CHOPA ZA CHADEMA RUKSA KALENGA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa maamuzi kuhusu hoja tatu kuu zilizowasilishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) yakiwamo madai ya matumizi ya helkopta, kuwatumia mawakala kutoka nje ya mkoa wa Iringa katika vituo vya kupigia kura Jimbo la Kalenga, ikisema chama chochote ruksa kufanya hivyo ilimradi hakivunji sheria za uchaguzi.
Juzi Chadema walitangaza kwamba itawatumia wabunge wake zaidi ya 42 pamoja na baadhi ya makada 1,000 kutoka mikoa mbalimbali kulinda kura katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo ambao utakafanyika Jumapili ijayo, huku CCM  walitangaza kwamba watawatumia makada vijana 260 kulinda wapigakura katika kata 13 za jimbo hilo.

Malalamiko hayo yalitolewa na Mratibu wa kampeni za CCM Jimbo la Kalenga, Miraj Mtaturu, wakati wa kikao cha NEC na wadau wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kalenga.

Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, akizungumza katika kikao hicho kilichowakutanisha wadau hao kutoka vyama vya siasa, polisi, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, waandishi wa habari na Idara ya Usalama, alisema NEC haitaingilia suala la vyama kuweka mawakala kutoka nje ya mkoa wa Iringa kwa kuwa suala hilo linaamuliwa na vyama vyenyewe.

NEC YAONYA KUHUSU SHAHADA
Kuhusu malalamiko ya vyama vyote kudai kwamba upande mwingine kununua shahada za wapiga kura kwa kutoa maelekezo kwa mawakala wa pembejeo za kilimo kutoa huduma hiyo kwa kukusanya vitambulisho vya kupigia kura, Jaji Lubuva aliamuru kwamba mawakala wote waliohodhi vitambulisho hivyo kuvirejesha mikononi mwa wapiga kura hao hadi kufikia leo jioni, vinginevyo NEC itachukua hatua dhidi ya wahusika, ingawa hakuzitaja.

Mkurugenzi wa Operesheni na Oganaizesheni wa Chadema, Benson Kigaila, alimweleza Jaji Lubuva kwamba CCM wanatumia vitambulisho hivyo kuwarubuni wapiga kura kwa kutoa mbolea ya ruzuku na pembejeo za kilimo kwa kutaka wananchi wawape kwanza kadi hizo ndipo wapate huduma wakati kampeni za uchaguzi huo zikiendelea.

CCM ikionyesha kukerwa na hoja hiyo na Mtaturu kumwambia Jaji Lubuva kuwa hilo si jambo jipya kufanyika katika halmashauri nyingi nchini, lakini ukweli ni kwamba hata  Chadema wanaolalamika pia wana mawakala wa pembejeo za kilimo ambao nao wanatoa huduma hiyo kwa kutanguliza maslahi yao mbele ikiwamo kuomba kwanza shahada hizo.

“Tukubaliane hapa kwamba wote ambao wanahusika kuchukua vitambulisho hivyo wavirejeshe ili wananchi hao wapate haki ya kupiga kura Jumapili kwa sababu hata wao Chadema wana mawakala wanaotoa huduma hiyo...Niwaombe wenzangu tukuabaliane katika hili na tuwape fursa wananchi wakatimize haki yao ya msingi,” alisema Mtaturu.

DAFTARI LA WAPIGAKURA
Aidha, vyama hivyo pia viliitaka NEC kutoa ufafanuzi kuhusu madai ya kuwapo kwa madaftari mawili ya wapiga kura ambayo yameibua mkanganyiko baina ya vyama vyote viwili na kusababisha hofu ya kutotendeka kwa haki Jumapili ijayo.

Jaji Lubuva, alisema daftari litakalotumika katika uchaguzi huo ni la mwaka 2010 na siyo daftari la mwaka 2014 ambalo linadaiwa kuboreshwa kutokana na mahitaji ya msingi, ikiwamo kuondoa majina ya watu waliopoteza maisha pamoja na majina ya wapiga kura yaliyo rudiwarudiwa.

“Naomba hili niliweke sawa, daftari litakalotumika siku hiyo ni lazima liwe la mwaka 2010 na si vinginevyo. Suala la vituo vya kupigia kura kuwekwa nyumbani kwa mabalozi au viongozi wanaohusishwa na itikadi ya CCM au kinginecho tumekataa na kimsingi vituo vyote hivyo tumeviondoa ...Tumeviweka maeneo ambayo kila mpigakura atakuwa huru kufanya uamuzi wake,” alisema Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Kalenga, Prudenciana Kisaka.

Kisaka alisema hadi sasa katika jimbo hilo hakuna mwananchi anayetembea umbali wa kilomita 35 kupiga kura isipokuwa kilomita 10 ambazo ofisi yake inatambua.

Katika mkutano huo, CCM waliitaka NEC itoe uamuzi wa kuzuia helkopta mbili za Chadema kutozunguka angani wakati uchaguzi huo ukiendelea kwa kuwa ni moja ya kampeni, lakini pia inawatia hofu wananchi wa Kalenga.

Akijibu hoja hiyo, Jaji Lubuva alisema kuwa NEC haitaki kuingilia suala hilo la helkopta kwa kuwa mwisho wa kampeni ni Jumamosi ijayo, hivyo atakayefanya kampeni siku  uchaguzi atachukuliwa hatua za kisheria.

“Hili la helkopta hatutaingilia sisi kama NEC isipokuwa nembo au sare ndilo tatizo na haturuhusu kabisa siku hiyo.

Lakini pia suala la wananchi kukaa mita 100 baada ya kupiga kura, sheria haisemi watu waondoke au wakae isipokuwa ikiwezekana vyama vyenyewe vitumie busara kuwataka wafuasi wao warejee majumbani,” alifafanua mjumbe wa NEC, Jaji Mstaafu John Mkwawa.

Wakati huo huo, Polisi Mkoa wa Iringa, imevionya vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo kutovitumia vikosi vyao vya ulinzi kwenye chama kwa kuwa jeshi hilo halitawatambua, badala yake itatumia nguvu kuwaondoa katika vituo vyote vya kupigia kura.

“Hivyo vikundi vya ulinzi vya chama chochote sijui ni Green Guard au Red Brigade havitakiwi katika eneo lolote lenye kituo cha kupigia kura siku hiyo ya uchaguzi. Nitaviondoa vyote na sitajali hiki ni cha chama gani, nawaombaeni sana visiwepo,” alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema jana kuwa ameamua kuongozana na wabunge wake 40 wa chama chake kwenda jimboni Kalenga kuzikabili saa 72 (siku tatu) zilizobaki kabla ya kufanyika kwa uchaguzi.

MBOWE AONYA WIZI WA KURA
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara wa kampeni kwenye uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, Mbowe alisema:

“Haki ya Mungu kitawaka wakijaribu kuiba kura, mimi na wabunge wangu 40 tumefungasha virago kuja hapa Kalenga. Tutalala nao na tutakula nao wapigakura wetu.”
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa