Halmashauri
ya wilaya ya Iringa imetakiwa kusimamia sheria ya Mazingira vizuri ili kuondoa
uharibifu wa mazingira katika bonde la mto Ruaha mkuu.
Agizo
hilo lilitolewa na mwenyekiti wa kikosi kazi namba tatu cha kunusuru ikolojia
ya mto Ruaha mkuu ambaye pia ni Katibu Tawala mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
wakati kikosi kazi hicho kilipokutana na timu ya menejimenti ya Halmashauri ya
wilaya ya Iringa jana.
Ayubu
alisema kuwa Halmashauri ya wilaya ya Iringa inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa
mazingira. “Ndugu zangu, sheria ya
Mazingira lazima isimamiwe ipasavyo. Katika kusimamia vizuri sheria hii wekeni
utaratibu mzuri wa kusimamia sheria hii kwa kuziimarisha kamati za mazingira
kuanzia ngazi za wilaya, kata na vijiji. Kamati hizi zikiimarishwa utekelezaji
wa sheria utakuwa mzuri na wenye kutoa matokeo mazuri zaidi” alisema Ayubu.
Aidha,
alizitaka kamati za Mazingira kutekeleza majukumu yake na kutoa taarifa za kazi
kwa mamlaka zinazohusika. Alisema kuwa utoaji wa taarifa utaziwezesha mamlaka
kuwa na picha kamili ya hali halisi ilivyo na kuwa na uelewa wa pamoja katika
kukabiliana na changamoto za kimazingira.
Ayubu
aliitaka Halmashauri hiyo kuelekeza miradi yote inayoanzishwa katika Halmashauri
hiyo kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira na
uhifadhi wa vyanzo vya maji. Alisema kuwa ipo miradi ambayo imekuwa ikianzishwa
pasipo kuwaelimisha wananchi juu ya utunzaji wa mazingira na kusababisha
uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.
Aidha,
aliitaka Halmashauri hiyo kuweka mikakati imara ya kutekeleza uhifadhi wa
mazingira. “Halmashauri ya wilaya ya
Iringa lazima muweke mikakati madhubuti inayotekeleza katika kusimamia
uendelevu wa agenda ya uhifadhi wa mazingira” alisema Ayubu.
Mwenyekiti
huyo alimtaka Mwanasheria wa Halmashauri kutoa elimu ya kina ya sheria ya
Mazingira na utekelezaji wake kwa kamati ya usalama ya wilaya ili kuiwezesha
inapotekeleza majukumu yake katika usimamizi na uhifadhi wa mazingira.
Kwa
upande wa afisa ardhi wa wilaya ya Iringa, Donald Mshani alisema kuwa
Halmashauri ya wilaya ya Iringa inakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira
kutoka na shughuli mbalimbali zikiwemo kilimo ndani ya mita 60 kutoka kingo za
mito na uingiaji wa mifugo mingi katika eneo ambalo halina uwezo wa kuihudumia.
Alisema kuwa katika kukabiliana na uharibifu huo, halmashauri ya wilaya ya
iringa imepanga kutekeleza mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyote
vinavyozunguka eneo la bonde la mto Ruaha mkuu ili uhifadhi wa mazingira uweze
kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na kuwa endelevu.
Awali
kaimu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa, Abel Mgimwa
alizitaja sababu zinazosababisha uharibifu wa mazingira katika Halmashauri hiyo
kuwa ni ukataji miti ovyo kwa lengo la kuongeza ukubwa wa mashamba na uchomaji
miti kwa ajili ya mkaa. Sababu nyingine alizitaja kuwa ni wafugaji wengi
kuingia maeneo ya ukanda wa chini katika Tarafa za Pawaga na Idodi na wananchi
kuanzisha mashamba mapya jambo linalosababisha kuondolewa kwa uoto wa asili.
Mgimwa
alisema kuwa changamoto hizo suluhisho lake ni mpango wa matumizi bora ya
ardhi. Aliongeza kuwa pamoja na mpango huo, sheria ndogo za vijiji kuhusu
hifadhi ya mazingira kwa vile vijiji ambavyo havina sheria hizo ili utekelezaji
wake uzingatiwe kikamilifu.
Halmashauri
ya wilaya ya Iringa ina jumla ya vijiji 133 kati ya vijiji hivyo, vijiji 61
ndivyo vimefanyiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.
0 comments:
Post a Comment