Na MatukiodaimaBlog
MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Iringa Ritta Kabati (CCM) amepinga hatua ya mstahiki meya wa Manispaa ya Iringa Bw Alex Kimbe kumsimamisha vikao vitatu diwani wa viti maalum Dolla Nziku (CCM) kwa madai ya kuvunja kanuni za baraza la madiwani.
Mbali ya kupinga uamuzi huo wa Meya mbunge huyo amepongeza uamuzi wa waziri wa ardhi , nyumba na maendeleo ya makazi Bw Wiliam Lukuvi kuzuia zoezi la Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuvunja nyumba za watumishi ambao wanadaiwa kuwa ni makada wa CCM.
Akizungumza na wanahabari jana mbunge Kabati alisema kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ambayo ipo chini ya Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA) imekuwa ikiongozwa kwa visasi jambo ambalo linaweza kurudisha nyuma maendeleo ya Halmashauri hiyo.
Kwani alisema kitendo cha Mstahiki meya huyo kumondoa ndani ya kikao cha baraza la madiwani diwani Nziku kwa kutumia vijana wa Chadema ni kosa la kikanuni na ni uvunjaji wa kanuni za vikao pia udhalilishaji kwa diwani huyo hivyo kumtaka mstahiki meya kumwomba radhi diwani huyo.
Alisema siku ya kikao ambacho diwani huyo alisimamishwa kosa lake lilikuwa ni kukosea kuvaa kofia wakati wa kikao kikiendelea na ndipo mstahiki meya huyo alipoamua kumfungia kuhudhuria vikao vya baraza la madiwani hata bila kupewa onyo ama kuitwa kwenye kikao cha maadili .
“Kosa alililitenda halikuwa la kumzuia kushiriki vikao hivyo bali lilikuwa ni kosa la kuonywa pekee ila mbaya zaidi meya amekuwa akiendesha baraza la madiwani kama mkutano wa Chadema maana ndani ya baraza la madiwani hata kama baraza hilo lipo chini ya Chadema ama CCM haikupaswa vijana wa chadema au CCM kutumika kumwondoa diwani ndani ya kikao cha kikanuni kwani huo si mkutano ama kikao cha chama “
Kabati alisema kuwa muda wa kutumikia adhabu ambao diwani huyo amepewa ni mkubwa na kutokana na kuwa diwani wa CCM kwa viti maalum kwenye Halmashauri hiyo yupo peke yake kumpa adhabu kubwa hivyo ni kuwanyima wanawake kupata mwakilishi wao ndani ya baraza hilo .
Diwani Nziku alisema kuwa kofia hiyo ilianguka bahati mbaya kutokana na nywele zake kuvaa nywele za bandia (wigi) hivyo kofia hiyo kushindwa kukaa kichwani na kuanguka bila kujua na baada ya kuelezwa hakukaidi aliivaa na ndipo meya huyo alipomtaka kutoka nje kwa kumpa adhabu ya kutoshiriki vikao vitatu .
“Sikukataa kutoka nje wakati nataka kusimama kwenye kiti ghafla meya aliita mgambo waje kunitoa ila kabla ya mgambo kufika vijana wa Chadema walinitoa kwa nguvu…..kweli nilidhalilishwa sana na kitendo hicho “
Katika hatua nyingine mbunge Kabati alipongea uamuzi wa waziri wa ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi Bw Lukuvi kuzuia ukandamizaji uliopangwa kufanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa chini ya Meya huyo kuagiza baadhi ya nyumba za Halmashauri wanazoishi watumishi wa umma hasa wale wanachama wa CCM kuvunjwa kwa madai ya kutaka kujenga mradi mkubwa .
Alisema kuwa kabla ya waziri kufika kuchukua uamuzi wa kusitisha zoezi hilo na kuzichukua nyumba hizo kutoka serikali za mitaa hadi serikali kuu kuwa tayari uongozi wa Manispaa ya Iringa umesha agiza makada hao wa CCM kuondoka katika nyumba hizo na kuanza kuvunja nyumba moja eneo la Makorongoni kitendo ambacho kilimfanya yeye mbunge kufika kupinga uamuzi huo.
Kwa upande wake Mstahiki meya wa Maispaa ya Iringa Bw Kimbe akijibu madai hayo alisema kuwa kwa suala la kupewa adhabu diwani huyo lipo kikanuni na hajafanya kwa matakwa yake ila amezingatia taratibu na kanuni zote zinazompasa kusimamia .
Bw Kimbe alisema kuwa kutokana na diwani huyo kuvunja kanuni nay eye akiwa ni msimamizi wa kanuni alimpa adhabu kwa mujibu wa kanuni na kuwa adhabu hiyo haina hata chembe ya chuki .
Pia meya huyo alikanusha madai ya mbunge Kabati kuwa zoezi la kuvunja nyumba hizo liliwalenga wana CCM kwani alisema zoezi hilo lililenga nyumba tano bila kuangalia anayeishi katika nyumba hizo ni mwanachama wa chama gani kwani kimsingi nyumba hizo zilikuwa ni mali ya Halmashauri kwa ajili ya watumishi wake na sababu ya kutaka kuzivunja ni kuongeza eneo la gulio katika eneo hilo .
Hata hivyo alipongeza hatua ya waziri mwenye dhamana ya ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi kumaliza mgogoro huo kwa nyumba hizo na nyingine zote katika Halmashauri za wilaya zaidi ya tano nchini kuchukuliwana serikali kuu.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment