Home » » VIONGOZI WA DINI WANAOMKOSOA RAIS DR MAGUFULI WASAJILI MAKANISA YAO KUWA VYAMA VYA SIASA - MGIMBA

VIONGOZI WA DINI WANAOMKOSOA RAIS DR MAGUFULI WASAJILI MAKANISA YAO KUWA VYAMA VYA SIASA - MGIMBA


Kada  Johnson Mgima  wakati  akiwa katika mchakato wa  kura  za maoni CCM Ludewa 

Na MatukiodaimaBlog
.......................................................................................
MWENYEKITI mstaafu  wa  umoja  wa vijana wa  kanisa la Anglikana nchini  Bw Johnson Mgimba azitaka taasisi  za  dini na viongozi wa  taasisi  hizo na  wale  wa vyama  vya  upinzani kuacha kufanya kazi  ya kuikosoa  serikali ya Rais Dr John Magufuli na badala  yake  kumuacha Rais aendelee kuwaletea maendeleo watanzania .

 Bw  Mgimba  ambaye  pia ni kada  wa  chama  cha mapinduzi (CCM) na  alipata  kuingia katika mchakato  wa  kura za maoni  ubunge   jimbo la  Ludewa katika uchaguzi  mkuu  wa  mwaka jana  aliyasema  hayo  wakati  akizungumza na  waandishi wa  habari  ofisini  kwake  kuhusiana na tabia  ya baadhi  ya  watu wakiwemo  viongozi wa  dini  kuacha  kufanya kazi  za  kuhubiri amani wamejigeuza  kuwa ni  wakosoaji wa   serikali jambo ambalo si jema .


" Hizi  taasisi  za  dini  na viongozi   wa makanisa wanakiwa kuacha kujishughulisha na masuala ya kisiasa na badala yake zitumike kuhubiri amani na upendo.. inasikitisha  sana  kuona viongozi  wa  dini  wanaacha  kuhubiri upendo na amani  wao  wanageuka  kuwa  wanasiasa  wa  kupandikiza  chuki na  kuikosoa  serikali kazi ambayo  si yao''.


Alisema kiongozi wa kiroho anapohubiri siasa badala ya neno   la Mungu ilihali anaowaongoza wana itikadi mbalimbali inaweza kuleta tafsiri tofauti na kuwakwaza wengine walio na itikati tofauti na kiongozi wao hata  wakati  mwingine makanisa  kujikuta  yanaliingiza Taifa  katika machafuko  badala ya amani .

"Hakuna mgogoro mgumu kuutatua kama ule unaotokana na imani za kidini na watanzania wanapaswa kuwa makini na viongozi wa aina hiyo ili kutovuruga amani ya nchi ambayo imejengwa kwa muda mrefu"

Kwani  alisema  kuwa makanisa  na taasisi za kidini zisiharibu na kuiaibisha madhabahu za Mungu kwa kuhubiri siasa na badala  yake kuwaacha wanasiasa wafanye ya  siasa  na   wao  wafanye  kazi yao  ya  kuliombea  Taifa na  kumuombea  Rais Dr Magufuli azidi  kuchapa  kazi zaidi .

Pasipo  kutaja  makanisa  hayo  wala  majina  ya  viongozi  wanaogeuza makanisa  ulingo  wa  siasa  alisema  hivi  sasa  imezuka  tabia ya  baadhi ya  wanasiasa   kuwatumia viongozi  wa dini  kueneza  chuki  zao  dhidi ya  serikali  kupitia viongozi  wachache wa dini  ambao wanashindwa  kutimiza  wajibu  wao wa  kiroho .


Alisema kama makanisa yanataka kufanya siasa basi yabadili usajili wao na kuwa vyama vya siasa ili kuweza kuifanya kazi ya siasa kwa uhuru na ufanisi zaidi  kuliko  kuendelea   kugeuza  makanisa  majukwaa ya  siasa .

Hivyo  alisema  wananchi  wote  wa Tanzania  bila  kujali itikadi  zao  za  vyama  wanapaswa  kuwapuuza viongozi wa  dini  wanaotumia makanisa vibaya na  badala  yake  kuzidi   kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli kwa mabadiliko makubwa anayoyafanya nchini .

Alisema hakukuwa na nidhamu ya kazi, watu walifanya mambo ya ovyo ovyo bila kujali na ili kurudisha hali kama ilivyokuwa miaka ya nyuma inatakiwa kuwa na mwenye matendo kama anavyofanya Dkt. Magufuli. kuwa kitendo cha kuwapa fursa vijana kwenye nafasi za uongozi ikiwemo ukuu wa mkoa, ukuu wa wilaya, ukurugenzi wa wilaya na nafasi nyingine serikalini.

Bw Mgimba alisema kinachotakiwa ni kwa vijana walioteuliwa kwenye nafasi mbalimbali wasimwangushe Rais na kuwatumikia wananchi kwa kuchangia kuleta maendeleo ya kweli kwao bila kujali itikadi wala dini zao.

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa