INAELEZWA kuwa migogoro ya ardhi itapungua katika maeneo mengi
nchini, baada ya wajumbe wa Kamati za Uamuzi za vjiji 10 vya wilaya za
Kilolo na Mufindi kupewa mafunzo ya haki za ardhi na utawala.
Ofisa Mradi wa Pelum Tanzania, Angole Rayson alisema mjini hapa juzi
kuwa, walibaini kuwa migogoro mingi inasababishwa na ukosefu wa mbinu
bora za kutatua migogoro ya ardhi pamoja na waamuzi kuwa na changamoto
ya ufahamu wa masuala yanayohusu haki za ardhi na utawala.
Kwa mujibu wa Rayson, mafunzo hayo yaliyolenga kuwaongezea uelewa
waamuzi hao kuhusu sheria za ardhi, haki za ardhi kwa wanawake na
makundi maalumu, yatasaidia kuhakikisha wananchi wanapata haki katika
masuala yote ya ardhi katika vijiji ambavyo waamuzi wake waliokwenye
Kamati za uamuzi wamepata mafunzo hayo.
Alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Ikuka, Mbigili, Mawala, Mawambala na
Masalali kwa upande wa wilaya ya Kilolo na Isaula, Magunguli, Makungu,
Usokami na Ugesa kwa upande wa wilaya ya Mufindi.
Mafunzo hayo yaliyofanywa kwa siku nne katika kila wilaya yametolewa
na mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yanayofanya kazi na
wakulima na wafugaji wadogo nchini Tanzania (Pelum Tanzania).
Alisema mafunzo hayo yanatolewa kupitia mradi wa kuhusisha jamii ya
vijijini katika uwajibikaji wa masuala ya ardhi ya kijiji unaojulikana
kwa jina la CEGO unaotekelezwa kwa uratibu wa mtandao huo na ufadhili
kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID).
Kwa maelezo yake, mradi huo wa miaka minne ulianza kutekelezwa mwaka
2013 ukihusisha pia vijiji vingine 20 vya wilaya nne katika mikoa ya
Morogro na Dodoma.
“Shughuli kuu za mradi huo ni kuongeza na kuimarisha uelewa wa haki
za ardhi kwa wananchi wa vijijini pamoja na viongozi wao kupitia
mafunzo, machapisho na mijadala mbalimbali,” alisema.
Akifunga mafunzo hayo wilayani Mufindi, Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Isaya Mbenje alisema ardhi ni mojawapo
ya rasilimali muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi.
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment