Home » » Serikali kuendelea kutoa dawa bure kwa wagonjwa wa ukimwi na kifua kikuu

Serikali kuendelea kutoa dawa bure kwa wagonjwa wa ukimwi na kifua kikuu

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Na: Lilian Lundo – MAELEZO
21/06/2016

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa sera yake ya kutoa dawa bure kwa wagonjwa wa kifua kikuu, ukimwi, mama wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka mitano inaendelea.

Hayo yamesemwa leo, mjini Dodoma na waziri wa wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu alipokuwa akitolea ufafanuzi wa swali la Mbunge wa Chalinze Mhe. Ridhiwani kikwete juu ya taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari kuwa utoaji wa dawa bure kwa makundi hayo ya watu umesitishwa na wanatakiwa kulipia.

“Hakuna mabadiliko yoyote katika sera ya kutoa dawa bure kwa wagonjwa wa ukimwi, kifua kikuu, mama wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka mitano, aidha nitaitaka hospitali ya Taifa ya Muhimbili inipatie maelezo juu ya taarifa hizo,” alisisitiza, Mhe. Ummy.

Wakati huo huo, naibu waziri wa wizara hiyo, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa wizara hiyo kwa kushirikiana na wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji wanaandaa mkakati wa kuongeza uzalishaji wa dawa nchini ili angalau kukidhi asilimia 60 ya mahitaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Aidha wizara hiyo pia iko katika mikakati ya kuunda chombo cha kusimamia gharama na bei zinazotozwa na vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa pamoja na bei za dawa na vifaa tiba ili kuthibiti uongezaji holela wa bei za dawa na vifaa tiba.

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa