Home » » KUWABAINI WATUMISHI HEWA PEKEE HAKUTOSHI.

KUWABAINI WATUMISHI HEWA PEKEE HAKUTOSHI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch. 


 Serikali imetakiwa kuchukua hatua dhidi ya vigogo waliosababisha kupotea kwa zaidi ya Sh5.7 bilioni kutokana na watumishi hewa 7,800 waliobainika.
Hayo yalisema jana na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiel Oluoch alipokuwa akizungumzia taarifa ya Serikali kuhusu mkakati wa kuwabaini watumishi hewa.
Juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Angela Kairuki alisema idadi kubwa ya watumishi hewa imegundulika kuanzia mwezi uliopita baada ya Rais John Magufuli kuagiza waondolewa kwenye orodha ya mishahara.
Oluoch alisema hoja si kutaja idadi na kiasi cha fedha zilizopotea, bali kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wakuu wa idara husika waliosababisha suala hilo.
“Hakuna ubishi kwamba watumishi hewa wanatokana na uzembe wa wasimamizi kwenye vitengo husika na kama ndivyo, waliosababisha yote haya wanajulikana na lazima wawajibishwe,” alisema.
Alisema ikiwa wakuu wa idara waliosababisha kuwapo watumishi hewa hawatachukuliwa hatua za kisheria, wizi huo utaendelea.
Aliitaka Serikali kuanika majina ya watumishi hewa waliopatikana, vituo vyao vya kazi na muda waliopewa mshahara wakati hawapo kazini.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba alisema matarajio yake ni kuona Serikali inachukua hatua stahiki kwa wote waliosababisha upotevu wa fedha hizo.
Alisema Serikali inao mfumo mzuri wa taarifa za watumishi waliofariki, kuugua kwa muda mrefu au kuacha kazi hivyo ni rahisi kuwajua walioshindwa kutekeleza wajibu wao ili wachukuliwe hatua za kinidhamu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Jimson Mhagaa alisema suala la kujitokeza watumishi hewa kila mara serikalini na katika taasisi zake kutamalizika iwapo wakuu wa vitengo husika watachukuliwa hatua.
Alisema ni ajabu kuona baadhi ya wafanyakazi wanaacha kazi au kufariki dunia lakini majina yao yanabaki katika orodha ya wanaopokea mishahara. Alisema suala hilo linaweza kuondolewa lakini inaonekana kuna watendaji wanaonufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na watumishi hao hewa, hivyo uamuzi unahitajika.

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa