WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua
huduma za madaktari bingwa katika Hospitali ya mkoa wa Iringa sambamba
na kampeni inayohamasisha utoaji kipaumbele cha huduma kwa wazee.
Huduma za madaktari hao zilizoanza kutolewa Aprili 25, mwaka huu
zinahusisha magonjwa ya ndani ya moyo, usingizi na magonjwa mahututi,
upasuaji, mfumo wa mkojo, watoto na magonjwa ya akinamama na uzazi.
Taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Robert Kasim
inaonesha tangu huduma za madaktari hao zianze kutolewa wagonjwa 245
wenye matatizo mbalimbali ya kiafya, wameonwa.
Dk Kasim alisema kati yao, 127 ni wanachama wa Mfuko wa Bima ya Afya
(NHIF) kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa huo na 118 ni wananchi wengine
ambao si wanachama wa mfuko huo.
Akizindua huduma na kampeni hiyo juzi, Mganga Mkuu wa Serikali,
Profesa Muhammad Kambi alisema mpango wa kupeleka madaktari bingwa
mikoani ni moja ya mipango itakayoendelezwa ili kuhakikisha kila
mwananchi anapata huduma bora za matibabu karibu na alipo.
“Huduma hizi tunazozitoa kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima
ya Afya tunazitoa hapa Iringa na zitaendelea kwa siku nyingine tano,
huduma hizi zinahitaji fedha nyingi. Fedha hizo ni zile zinazochangwa na
wanachama wa mfuko huo na zile za wanachama wa Mfuko wa Afya ya Jamii,”
alisema.
Profesa Kambi alimweleza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwa, pamoja na
huduma hizo kupelekwa mkoani humo, takwimu zinaonesha wananchi wengi
bado hawajachangamkia kujiunga na mifuko hiyo kwa kuzingatia taratibu
mbalimbali za uchangiaji.
Akizungumzia huduma kwa wazee, alisema kwa kuwa wizara hiyo imepewa
jukumu la kusimamia masuala ya wazee, wameona waanze kuwaenzi kwa
kuhakikisha wanapata kipaumbele cha huduma za matibabu.
Awali Mkurugenzi wa Tiba na Ushauri wa Kiufundi wa NHIF, Frank Lakey
alisema msingi mkubwa wa mpango huo ni dhamira ya NHIF ya kutoa huduma
bora za matibabu kwa usawa kwa wanachama wake wote na wananchi kwa
kuzingatia mahitaji yao, bila kujali hadhi zao, kiwango cha uchangiaji
au maeneo ya kijiografia wanayoishi.
“Tangu kuanza kwa mpango huu mwaka 2013, mikoa 14 imefikiwa hadi sasa
ambako wagonjwa 11,612 walipata huduma na kati yao 392 walifanyiwa
upasuaji wa aina mbalimbali,” alisema kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu
wa NHIF, Michael Mhando.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu aliipongeza
wizara na NHIF kwa kubuni mpango huo unaosaidia kupunguza gharama kwa
wagonjwa.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment