Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa imewahukumu kwenda jela miaka
mitano au kulipa faini ya Sh milioni 1.5 kila mmoja, dereva Hansi
Mwakyoma (28) na utingo wake, Alex Adam (32) baada ya kukamatwa na
kukiri kusafirisha wahamiaji wasio na vibali 83 kutoka Ethiopia.
Wahamiaji hao wamehukumiwa kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya Sh milioni moja kila mmoja.
Kwa kutumia gari aina ya Scania lenye namba za usajili T478 DFE, mali
ya Flora Mwambenja wa Mbeya, Januari 16, mwaka huu, dereva huyo na
utingo wake, walikamatwa katika kijiji cha Ruaha Mbuyuni wilayani Kilolo
Barabara Kuu ya Iringa - Mbeya, wakiwasafirisha watu hao kwenda Kyela
mpakani mwa Tanzania na Malawi.
Akitoa hukumu hiyo juzi, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Iringa,
Andrew Scout alisema ameridhika na maelezo yaliyotolea na Wakili wa
Serikali na vielelezo, likiwamo gari lililotumiwa na watuhumiwa hao
kusafirisha watu hao kutoka Kongowe, Dar es Salaam kwenda Kyela mkoani
Mbeya.
Baada ya kusoma hukumu hiyo, baadhi ya raia hao wa Ethiopia waliangua
kilio mahakamani hapo na kusababisha watu waliokuwa karibu na jengo
hilo, kusogea ili kujionea kulikoni.
Mkalimani wa wahamiaji hao, ambao hawazungumzi Kiingereza wala
Kiswahili zaidi ya lugha ya kwao, Emmanuel Mtaltisili ambaye ni
mtangazaji wa kituo cha redio ya Ebony FM cha mjini Iringa alisema;
“walichokitarajia wahamiaji hao ni kupewa hukumu ya kurudishwa kwao
baada ya kukiri kosa hilo.”
Awali akisoma maelezo ya kosa la watuhumiwa hao baada ya wote kukiri
kosa mbele ya mahakama hiyo, Wakili wa Serikali kutoka Idara ya
Uhamiaji, Godfrey Ngwijo alisema ilikuwa Januri 16, mwaka huu katika
eneo la Ruaha Mbuyuni watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa ndani ya gari
hilo lenye bodi lililofunikwa, wakisafiri kutoka Kongowe kwenda Malawi
kinyume cha Sheria ya Uhamiaji ya Mwaka 2002 iliyofanyiwa Marejeo mwaka
2015.
Alisema katika tarehe isiyojulikana, watuhumiwa 83 raia wa Ethiopia
waliingia nchini kwa kutumia njia zisizo halali na kwenda Dar es Salaam,
walikoanzia safari yao ya kwenda Kyela mkoani Mbeya ili waingie nchini
Malawi.
CHANZO; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment