Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mary Shangali amesema
Mahakama kwa kushirikiana na wadau wake wengine ina jukumu la kutoa
elimu ya sheria kwa umma ili uelewe taratibu za msingi katika
upatikanaji wa haki mahakamani.
Akifungua rasmi Wiki ya utoaji wa elimu ya Sheria kwa umma katika
viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa juzi, Jaji Shangali alisema
Mahakama ya Tanzania imeazimia kuweka utaratibu wa kuadhimisha Siku ya
Sheria nchini kwa kutanguliwa na Wiki ya elimu ya Sheria kwa wananchi.
Alisema utaratibu huo ulioanza jana, unawahusisha wadau wote katika
sekta ya utoaji haki wakiwemo mawakili wa serikali, mawakili wa
kujitegemea, Polisi, Magereza, Takukuru na vyama vya msaada wa kisheria.
Mbali na kutumia vituo vya redio kutoa elimu hiyo, Jaji Shangali
alivitaja vituo vitakavyotumika pia kutoa elimu hiyo kuwa ni pamoja na
kwenye magereza yote ya kanda ya Iringa, Jumba la Maendeleo mjini
Iringa, Mahakama Kuu na viwanja vya manispaa.
Alisema wananchi wengi hasa wale wa vijijini watanufaika na utaratibu
huo kwa kuzingatia kwamba wengi wao hawajui sheria na taratibu
zinazotumika katika utoaji wa haki.
“Tunategemea wananchi wengi watajitokeza katika vituo hivyo ili
wapate uelewa wa huduma zitolewazo na Mahakama na elimu ya Sheria kwa
ujumla,” alisema Jaji Shangali.
CHANZO; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment