Home » » IRINGA YAJISTOSHELEZA KWA CHAKULA.

IRINGA YAJISTOSHELEZA KWA CHAKULA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
MKOA wa Iringa unaelezwa kujitosheleza kwa chakula kutokana na mavuno ya tani 1,291,070 za nafaka, mikunde na mizizi kwa msimu wa mwaka 2014/15.
Hayo yalielezwa hivi karibuni na Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Sekta za Uzalishaji, Fikira Kisimba wakati akitoa taarifa ya mandeleo ya kilimo kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana kwa Kamati ya Ushauri ya Mkoa. Kisimba alisema nafaka pekee zilizovunwa katika msimu huo ni tani 963,981, mikunde tani 135,352 na mizizi ni tani 191,737.
Kwa mujibu wake, mkoa huu ulihitaji tani 346,989 za nafaka na mikunde ili kutosheleza wakazi wake kwa mwaka mzima, hivyo kutokana na mavuno hayo, unajitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ya tani 651,691 za nafaka.
“Lakini pamoja na kuwa na ziada ya chakula, yapo baadhi ya maeneo katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa na Kilolo yenye upungufu wa chakula,”alisema na kuyataja maeneo hayo kuwa ni tarafa za Isimani, Pawaga, Idodi, Mahenge na Mazombe.
Katibu Tawala Msaidizi huyo alieleza sababu za upungufu huo wa chakula katika maeneo hayo kuwa ni ukame uliosababisha mavuno chini ya asilimia 30.
Akielezea jitihada zilizofanywa na mkoa, Kisimba alizitaja kuwa ni kupeleka maombi ya chakula katika Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa pamoja na kuomba kibali cha wafanyabiashara wenye mashine za kusaga kwenye maeneo ya waathirika ili kununua mahindi kutoka kwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA - Makambako) ili wauze unga kwa waathirika wa njaa kwa bei nafuu.
Agosti mwaka jana, mkoa ulipata kibali cha kununua tani 100 za mahindi kwa ajili ya mkoa huu.
“Novemba mwaka jana tulipata kibali cha kuchukua tani 400 za mahindi ambapo, tani 320 zilikuwa ni za Halmashauri ya wilaya ya Iringa na tani 80 kwa ajili ya Halmashauri ya wilaya ya kilolo. Desemba mwaka huo mkoa ulipata pia kibali cha kununua tani 350 za mahindi ambapo 200 zilikuwa ni za Halmashauri ya wilaya ya Iringa na tani 150 za Halmashauri ya wilaya ya Kilolo,” alisema Kisimba.
CHANZO ; HABARI LEO.

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa