Home » » MILIONI 198/- ZASAIDIA KAYA MASKINI KILOLO.

MILIONI 198/- ZASAIDIA KAYA MASKINI KILOLO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
KAYA masikini 6,490 za vijiji 70 vya wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, zimepata malipo ya nne ya zaidi ya Sh milioni 198.5 zitakazoziwezesha kuongeza kipato, fursa na uwezo wa kugharimia mahitaji yao muhimu.
Fedha hizo zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) zinazifanya kaya hizo ziwe zimepata zaidi ya Sh milioni 800 tangu mpango huo uanze Julai mwaka jana.
“Zaidi ya Sh milioni 800 zimeletwa wilayani Kilolo kwa ajili ya kuzinusuru kaya hizo, ni matarajio yetu fedha hizo zitasaidia kubadili maisha ya watu wa Kilolo kama ilivyokusudiwa,” alisema Mratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Kilolo, Venance Mwaikambo wakati wa shughuli ya kugawa fedha hizo.
Mwaikambo alisema litakuwa jambo la kushangaza kama baadhi ya kaya zinazonufaika na mpango huo zitaonekana hazijabadilika.
“Serikali haijaleta fedha hizi kama zawadi inataka mtoke kutoka hatua moja mwende hatua nyingine,” alisema huku baadhi ya kaya zikikiri kuanzisha miradi midogo ya ufugaji na kilimo kwa kutumia fedha hizo.
Alisema ni makosa fedha hizo kutumika kwa starehe au michango mbalimbali inayohimizwa katika maeneo wanayotoka.
Kwa kupitia mpango huo, Mwaikambo alisema kaya hizo zina fursa ya kuboresha maisha yao kwa kutumia akiba ya fedha wanayoweza kuipata kutoka katika Sh 20,000 na zaidi ya Sh 70,000 wanazopata kila baada ya miezi miwili.
Ofisa Ushauri na Ufuatiliaji wa Tasaf wilayani Kilolo, Happy Mpuya alisema serikali kwa kupitia mpango huo inatoa ruzuku ya msingi na ya masharti nafuu kwa kaya masikini ili kugharimia mahitaji ya msingi ikiwemo elimu, afya na maji.
Mpuya alisema ruzuku ya msingi inatolewa kwa kila kaya iliyoandikishwa kwenye mpango ili kugharimia mahitaji hayo ya msingi na ruzuku ya masharti nafuu inatolewa kwa kaya masikini zenye watoto wenye umri wa kwenda shule na kliniki.
“Mpango unalenga pia kutoa ajira ya muda kwa kaya hizo na zenye watu wenye uwezo wa kufanya kazi wakati wa kipindi cha hali na majanga mbalimbali kama vile ukame na mafuriko,” alisema.
Alisema kaya zitakazobainika kuzitumia fedha hizo kinyume na malengo hayo zitaondolewa katika mpango kama masharti ya mpango yanavyotaka.
Mmoja wa walengwa wa mpango huo, Lickson Chambaga (70) wa kijiji cha Luganga aliyepata jumla ya Sh 80,000 toka Julai mwaka jana alisema; “kwa kupitia akiba ya Sh 30,000 niliyojiwekea, nilinunua kuku tetea wawili na jogoo mmoja. Hivi sasa nina kuku 14 ambao watanipa faida kama nitawauza baada ya kukua vizuri.”
 CHANZO ; HABARI LEO.

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa