Home » » Uandikishaji wa BVR wakwama leo kuanza Iringa.

Uandikishaji wa BVR wakwama leo kuanza Iringa.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Biometric Voters Registration (BRV).
Uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura kwa kutumia mfumo mpya wa Biometric Voter Registration (BVR) umekwama kuanza mkoani Iringa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kucheleweshwa kwa vifaa.
 
Akizungumza na NIPASHE jana kwa niaba ya Ofisa Uandikishaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Gabriel Msunza, alisema uandikishaji ulipangwa kuanza leo,  lakini kutokana na changamoto hiyo wameamua kusogeza mbele hadi Jumatano ijayo.
 
Msunza alisema hadi sasa wamepokea BVR 39 na vifaa hivyo ni kwa ajili ya mafunzo kwa waandishaji wasaidizi na kwamba wanasubiri utaratibu mwingine kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).
 
“Tunawasubiri tume leo (jana) wakishafika tutakaa nao na kujadili na baadaye watatupatia tarehe rasmi ya kuanza uandikishaji baada ya waandikishaji wasaidizi kupata mafunzo ya namna  ya kutumia mashine hizo.
 
 Alisema Manispaa ya Iringa wanatarajia kuandikisha zaidi ya wapiga kura 79,089.
 
Wakati huo huo, Wilaya ya Lindi Vijijini, mkoani hapa, imepokea vifaa vya uandikishaji wa wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo wa kielektroniki wa  Biometric Voters Registration (BRV).
 
Vifaa hivyo vitatumika kuandikisha wapigakura kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Hayo yameelezwa na ofisa Uchaguzi wa wilaya hiyo, Musa Nkolovigawa, alipokuwa akitoa maelezo wakati wa semina ya mafunzo ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la wapigakura. Nkolovigawa alivitaja vifaa vilivyopokelewa kuwa ni BRV kiti 66, stendi za kamera, bahasha, kofia, tisheti, mabegi ya kubebea vifaa na karatasi zitakazotumika kujaza taarifa za mtu atakayefika kituoni kujiandikisha.
 
Alisema kupokelewa kwa vifaa hivyo ni moja ya ushahidi kuwa kazi ya uboreshaji wa daftari hilo itaanza wiki hii kama ilivyopangwa.
Nkolovigawa alisema kazi ya uandikishaji imepangwa kuanza leo kwa utaratibu wa kanda nne, ikimaanisha kata zote za majimbo yote mawili ya Mtama na Mchinga.
 
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Yahaya Nawanda, aliwataka maofisa waandikishaji ngazi ya kata wanakuwa makini kutokana na uandikishaji kuwa ni suala nyeti na muhimu kwa kwa mustakabali wa Taifa. Uandikishaji wa wapigakura katika Halmashauri ya wilaya hiyo utaanza leo na kukamilika Mei 28, mwaka huu.
 
Imeandikwa na George Tarimo, Friday Simbaya, Iringa na Said  Hamdani, Lindi
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa