Home » » NEWS: 42 WAPOTEZA MAISHA MAFINGA KWA AJALI

NEWS: 42 WAPOTEZA MAISHA MAFINGA KWA AJALI

 Basi la Majinja Express likiwa limeharibika vibaya baada ya kuangukiwa na kontena katika ajali iliyotokea nje kidogo ya mji wa Mafinga jana eneo la Changalawe barabara kuu ya Iringa Mbeya.
Msululu wa magari ukiwa unasubiri kuondolewa kwa maiti katika eneo la ajali (Picha zote na Denis Mlowe).




NA DENIS MLOWE, MUFINDI


HUZUNI na majonzi yametawala katika mji mdogo wa Mafinga baada ya ajali mbaya ya basi la abiria la Majinja Express lilokuwa likitokea jijini Mbeya kuelekea Dar Es salaam kugongana uso kwa uso na kisha kudondokewa na Kontena na kusababisha watu 42 kufariki dunia katika ajali iliyotokea eneo la Changarawe barabara kuu ya Iringa kwenda Mbeya.
 


Ajali hiyo ambayo hatazamiki mara mbili imetokea majira ya 3.30 asubuhi km 5 kutoka mjini Mafinga kwa lori lenye namba T689 APJ likiendeshwa na dereva aliyejulikana kwa jina la Maka Sebastian (26)mali ya CIPEX Company kwa kontena kuangukia basi la Majinja Express lenye namba T438 CDE likiendesha na dereva Baraka Gabriel (37).
 


Katika ajali hiyo waliofariki dunia papo hapo walikuwa 37 na watano wamefariki wakiwa hospitali ya wilaya ya Mufindi na inasemekana wengi wao ni wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam waliokuwa wakitokea jijini Mbeya kati ya hao walofariki ni wanaume 32 wanawake 7, watoto 3 na majeruhi 22.


Mmoja wa abiria wa basi hilo,Musa Mwasege akisimulia chanzo cha ajali hiyo alisema kuwa chanzo ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa  basi alilopanda kwa kuwa katika mwendo kasi licha ya ubovu wa barabara hiyo kuwa na mashimo mengi yanayosababisha ajali.


“Sehemu iliyotokea ajali kwa kweli ni mbovu hivyo dereva wetu baada ya kupunguza mwendo akawa anazidi kuongeza na kutumbukia katika shimo na kusababisha kugonga uso kwa uso na roli hilo na kisha kontena kutuangukia baada ya hapo sikutambua lolote hadi nilipofika hospitali” alisema.


Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza akizungumza katika eneo la ajali alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni ubovu uliokithiri wa barabara hiyo na ni tukio la kuhuzunisha sana kwa wa watanzania na kuagiza wakala wa barabara kuanza matengenezo ya barabara hiyo.


Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, amekiri kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa chanzo cha ajali ni ubovu wa barabara kutokana kuwa na mashimo mengi.


“Hapa tusitafute mchawi nani katika hii ajali chanzo kikubwa ni ubovu wa barabara hivyo ni jukumu la mamlaka husika kurekebisha tatizo la barabara.” Alisema.


Kamanda Mungi aliwataja abiria waliokuwemo katika basi hilo kuwa ni Esta Emanuel Lusekelo, Jerimiah Wakison, Doto Katuga, Diga Solomon, Theresia Kaminyage, Frank Chiwango, Luteni Sanga, Alfred Sanga, Juliana Bukuku, Esta Fide, Paulina Justin.


Wengine ni Catherine Mwajengi, Zira Kasambala, Rebeka Kasambala, Mbamba Ipyana, Dulile Kambala, Frank Mbaule, Mustapha Ramadhan, Bwana Mussa, Shadrak Msigwa, Mathias Justin, na aliyejulikana kwa jina moja la Elias. 


Naye mganga mkuu mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Mufindi Boaz Mnenegwa alikiri kupokea maiti 37 na majeruhi 22 zilizotokana na ajali hiyo na kusema kuwa majeruhi watano walifariki mara baada kufikishwa kituoni hapo.

Alisema kuwa kutokana ufinyu wa nafasi katika chumba cha kulaza maiti hospitalini hapo maiti 32 zilisafirishwa kuelekea katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa na majeruhi waliokuwa mahututi wawili wote wa kiume walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa  katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa.
 Chanzo: Jiachie Blog

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa