Home » » VURUGU HIZI NI UKOSEFU WA NIDHAMU POLISI

VURUGU HIZI NI UKOSEFU WA NIDHAMU POLISI

Ukizisoma Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (Police General Orders) au kwa kifupi PGO, zimetoa mwongozo mzuri wa namna ya kutekeleza majukumu ya kipolisi. Lakini kubwa zaidi ni usimamizi wa nidhamu kwa askari.
Tumeona tuanze kujenga hoja ya rai yetu kwa kutumia PGO kutokana na mlolongo wa matukio yanayolikumba jeshi hilo, ikiwamo tukio la juzi katika mji mdogo wa Ilula wilayani Kilolo mkoani Iringa.
Ni mwendelezo wa matukio ya kusikitisha ambapo sasa wananchi wamefikia hatua mbaya ya kuharibu mali za jeshi hilo, kwa kuchoma moto vituo vya polisi na magari yao.
Uvamizi na uharibifu wa mali za Jeshi la Polisi unaofanywa na wananchi siyo wa kupongezwa, ni kichaa tu ndiye atawaunga mkono wananchi hao. Hatuna haja ya kuorodhesha matukio hayo sababu yanafahamika.
Miaka ya nyuma polisi walikuwa wakiheshimika sana na siyo hivyo pekee hata woga kwa polisi ulikuwa mkubwa. Kipindi hicho watu walitii sheria bila shuruti, kwa sababu polisi wenyewe walitii na kuitekeleza kwa vitendo PGO bila shuruti.
Ripoti nyingi za utafiti zinawataja polisi kwamba wako nafasi za juu kwa kuomba rushwa, kwa ujumla yanayotokea ni kwa sababu nidhamu ndani ya Jeshi la Polisi haipo, ndiyo maana wananchi hawana heshima wala woga kwa polisi.
Siku hizi ni kawaida mtuhumiwa au mhalifu kubishana na polisi, tena wanapatana hata kiasi cha rushwa. Mengi yanazungumzwa, askari kukaa kituo kimoja kwa muda mrefu hadi anazoeana na wahalifu, kuishi uraiani, lakini kubwa zaidi ni nidhamu.
Siku hizi, askari hawafuati misingi ya upolisi kama ilivyo kwenye PGO. Misingi inasema, kwa mfano, askari hatakiwi kuacha lindo hadi mwenzake afike lakini siku hizi askari anaacha lindo kabla mwenzake hajafika.
Ni jambo la kawaida siku hizi kuona askari akiingia kazini huku amelewa. Lakini kwenye PGO unaambiwa kabla askari hajaingia lindoni ni lazima akaguliwe lakini siku hizi hilo halifanyiki.
Wakati wa kumtafuta mrithi wa IGP Said Mwema gazeti moja lilitabiri maofisa watatu, Thobias Andengenye, Ernest Mangu na Diwani Athumani. Lakini sifa pekee ya Mangu ilikuwa ni usimamizi mzuri wa PGO.
Utabiri huo ulikuwa kweli kwa Mangu na baada ya uteuzi zilitajwa sifa zilizompa alama nyingi kwenye kupata wadhifa wake huo ikiwamo namna anavyofahamika kwa usimamizi wake wa PGO, hasa usimamizi wa maadili ya uaskari.
Tungependa kusisitiza kuwa kaulimbiu ya “Nidhamu ni nguzo thabiti katika utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi”, iliyotumika kwenye mkutano wa Maofisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi uliofanyika mkoani Dodoma mwezi uliopita iendelezwe kwa vitendo. Bila polisi wenyewe nidhamu hakuna atakaye waheshimu wala kuwaogopa.
Sisi tunaamini kama nidhamu ndani ya Jeshi la Polisi itasimamiwa ipasavyo, askari wakaheshimu haki za raia, wakalinda mali za raia, wakaacha kuwa wanasiasa na wakatenda haki, heshima waliyokuwa wakiipata kwa wananchi itarejea.

Rai yetu kwa IGP Mangu na Naibu IGP Abdulrahmani Kaniki hakikisheni mnarejesha nidhamu ndani ya Jeshi la Polisi ili wananchi wapate kuwaheshimu. Kauli ya kutii sheria bila shuruti, pia ifanye kazi kwa polisi nao watii PGO bila shuruti.
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa