Home » » WASOMI WAZUNGUMZIA MATUMIZI YA PESA URAIS.

WASOMI WAZUNGUMZIA MATUMIZI YA PESA URAIS.

Mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru.
Baadhi ya wasomi wamezungumzia matumizi ya fedha kwa wagombea urais na kuleza kuwa hayakubaliki huku wengine wakidai kuwa wagombea wote wa CCM walioonyesha nia ya kuwania urais wanatumia fedha, hivyo watafute namna nyingine ya kuwachuja na siyo kwa kiwango cha fedha wanachotoa.

Kauli za wasomi hao zinatokana na kauli ya mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru, aliyesema kuwa hakuna aliye msafi kati ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliojitokeza kutaka kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Akihojiwa katika kipindi cha ‘Kumekucha’ kilichorushwa hewani na kituo cha Independent Television (ITV) juzi asubuhi, alisema makada wote wanatumia fedha na kufanya faulo mbalimbali katika kusaka nafasi hiyo kinyume cha maadili.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Bukoba, Dk. Azavel Rwaitama, alisema CCM ilipofika ni kweli kuwa fedha inatumika kwenye chaguzi mbalimbali, hivyo kitafute namna nyingine ya kuwashughulikia wagombea na siyo kutumia kigezo cha fedha kwa kuwa hadi sasa hakuna mgombea aliyeonyesha nia ya kugombea ambaye hatoi fedha.

“Kauli ya Kingunge inalenga kuwakumbusha wasitafute mtu anayesambaza fedha kama kosa, bali waangalie mapungufu mengine,” alisema na kuongeza:

“Haisaidii, wakae chini na kuangalia vigezo vya hao wanaotoa fedha kwa kuwa hakuna ambaye hajagawa fedha…wasiingie kwenye matatizo na watu kwa kutafuta waliogawa fedha, waangalie mambo mengine.”

Dk. Rwaitama alisema kwa tafsiri ya haraka, chama hicho tawala kilipofika siyo rahisi kuwa na mgombea anayepata nafasi bila kutumia fedha.

“Nilichokiona ndani ya kauli ya Kingunge, lengo lake ni kuionya CCM. Ni jambo la maana, wamsikilize, lakini pia ni ushahidi kuwa CCM tuachane nayo na kwenda kuangalia upande mwingine,” alibainisha.

Naye Mhadhiri wa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema kauli ya Kingunge inatafsiri mbalimbali ikiwamo matumizi ya fedha kwa wagombea ambayo ni hatari kwa mustakabali wa Chama.

Alisema kwa kawaida mgombea anayesimamishwa na chama ndicho kinapaswa kugharimia kampeni na hakuna anayeruhusiwa kutumia fedha zake binafsi kwani ni kinyume cha maadili na nidhamu.

“Tunataka chama kigharimie kampeni na kitoe ruzuku, tungekuwa na mgombea binafsi angejigharimia, lakini kwa anayepitia kwenye chama ni lazima matumizi yake gharimiwe na chama,” alisema na kuongeza:

“Kama akitoa fedha zake mfukoni zinatoka wapi unazigawaje, wewe ni nani kugawa pesa, fedha ina heshima yake…akiruhusiwa kutumia fedha zake chama hakitaweza kumdhibiti, anakiweka chama rehani.”

Alisema chama makini lazima kigharimie kampeni za uchaguzi na kwamba kauli hiyo haikutazama muktadha wa kampeni za Tanzania.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), Prof. Mwesiga Baregu, alisema kama makada wote walioonyesha nia wanatumia fedha ni wazi kuwa hakuna anayestahili kugombea.

“Hatuwezi kupata rais bora kwa matumizi ya pesa, anunue urais kwa mazingira haya CCM haina mgombea wa kuwa rais, Watanzania watafute mtu mwingine,” alisema.

Hata hivyo, NIPASHE ilimtafuta Mhadhiri wa UDSM, Dk. Bashiru Ally, alisema hawezi kuzungumzia suala la mbio za urais.

Naye, Profesa Mkumbo Kitila, wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu (Duce) cha UDSM, alipoulizwa, alisema yupo kwenye mkutano na kutaka atumiwe ujumbe mfupi, ambao licha ya kutumiwa, haukujibiwa hadi tunakwenda mtamboni simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

MAKADA WALIOTANGAZA NIA
Makada wa CCM waliotangaza nia na wanaotajwa kuwania urais kupitia chama hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Mbunge wa Nzega, Dk. Hamis Kigwangalla; Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.

Wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya juu kuliko zote nchini ni Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na mawaziri  wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.

Wengine ni Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Prof. Mark Mwandosya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira.

Kati ya makada hao, sita waliwahi kuitwa na Kamati Ndogo ya Nidhamu iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, na kuwahoji kwa tuhuma za kuanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao kabla ya wakati.

Baada ya mahojiano hayo, Februari, mwaka jana, Kamati Kuu (CC) ya CCM ilitangaza uamuzi mzito dhidi ya makada wake hao baada ya kutiwa hatiani, kwa kuwafungia kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa miezi 12, huku pia wakiwa chini ya uangalizi.

Makada hao ni pamoja na Sumaye, Lowassa, Membe, Wasira, Ngeleja na Makamba, ambao mwezi ujao, wanatarajiwa kukamilisha kutumikia kifungo chao huku chama kikisubiriwa kutangaza hatma yao wakati wowote kuanzia wiki hii baada ya kipindi cha uangalizi kupita.

KABLA YA VYAMA VINGI HALI IKOJE
Miaka ya nyuma wakati wa kampeni za uchaguzi wagombea walibebwa kwenye gari moja na kupelekwa kwenye maeneo ya kupiga kampeni.
Baada ya mfumo wa vyama vingi, kipindi cha kura za maoni wagombea hutumia gari moja kwenye kwenye maeneo mbalimbali kufanya kampeni za kupitishwa ndani ya chama.
CHANZO: NIPASHE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa