Home » » WAKANDARASI IRINGA WAONYWA

WAKANDARASI IRINGA WAONYWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAKANDARASI mkoani hapa wametakiwa kufanya kazi  zao kwa kuzingatia sheria, ubora na ujuzi unaokidhi viwango vya kimataifa huku wakitanguliza uzalendo katika kutekeleza miradi ya maendeleo wanayokabidhiwa na halmashauri husika.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashuri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa, wakati wa kusaini mikataba mbalimbali kwa kampuni za ukandarasi 17 mkoani hapa, kwa ajili ya kutekeleza miradi ya barabara na madaraja inayotekelezwa na mfuko wa barabara na halmashauri ya Wilaya hiyo katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mwishoni mwa wiki.
Mhapa, alisema wakandarasi wengi wanashindwa kufanya kazi kwa vigezo vinavyotakiwa na kusababisha miradi mingi kujengwa chini ya viwango, kutokana na baadhi yao kutotimiza majukumu yao ipasavyo.
“Nakerwa na kitendo cha wakandarasi kuzifanya halmashauri kama shamba la bibi la kuchuma fedha na kutekeleza miradi ya madudu… nataka niwaambieni mkandarasi yoyote atakayeshindwa kufanya kazi yake kwa ubora unaotakiwa, naomba kabisa asije kuomba tenda hapa kwetu na hata akipitishwa na viongozi, mimi kama Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa siwezi kusaini kama nitaona jina lake au la kampuni yake,” alisema Mhapa.
Aliwataka wakandarasi waliofanikiwa kutimiza vigezo katika halmashauri hiyo na kupata tenda hizo, kuwapa ajira wananchi wanaoishi mazingira ya miradi inayotekelezwa na kujitambulisha kwa wanakijiji husika, kutoa ushirikiano na kubandika matangazo yanayohusu mradi na onyo kwa ugonjwa wa ukimwi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Pudenciana Kisaka, aliwaasa wakandarasi kuzingatia mkataba na kumaliza kwa wakati muafaka kulingana na mikataba waliyosaini, la sivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa na kutopewa mikataba mingine.
Alibainisha kuwa, miradi ya ujenzi wa barabara na madaraja utagharimu sh bilioni 1.6 ambako itakarabati sehemu korofi, mifereji na matengenezo ya kawaida ya barabara.

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa