Home » » WAASWA KUEPUKA VISHAWISHI VYA NGONO

WAASWA KUEPUKA VISHAWISHI VYA NGONO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WANAFUNZI waliohitimu darasa la saba shule ya Msingi Tagamenda Kalenga Iringa Vijijini wameaswa kudumisha nidhamu, maadili na kuepuka vishawishi vya ngono za umri mdogo badala yake wazingatie masomo ya Sekondari ili kufikia ndoto za maisha yao.
Hayo yalisemwa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), Patrick Myovela, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 34 ya shule hiyo yaliyofanyika juzi, akimwakilisha Mbunge wa Kalenga, Godfrey Mgimwa.
Alisema wahitimu hao wanahitaji kuzingatia afya kwa faida ya familia na taifa kwa ujumla kwa siku za baadaye, ili kuwa na taifa lenye wachapakazi bora na wenye afya njema, kwani janga la ukimwi limezidi kuwa tishio hasa kwa rika la vijana.
Myovela, alisema taifa bora linahitaji vijana walio na elimu iliyo na msingi imara kutoka awali hadi chuo kikuu katika mazingira ambayo walimu na wanafunzi wanawezeshwa kukabiliana na changamoto wanazokumbana naz na kuzifanyia kazi katika kuwapatia elimu wanafunzi.
Aidha, aliwaasa wazazi kutokubali kutengeneza mazingira ya mabinti wanaohitimu darasa la saba kwenda kufanya kazi za uyaya jijini Dar es Salaam kwa misingi ya tamaa ya fedha na kuwakumbusha kuwa, kuna unyanyasaji unaofanyika dhidi ya watoto wao na hata kufukuzwa kazi na kisha kujiingiza katika janga la uchangudoa.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Beatus Shayo, alisema shule hiyo ina changamoto ya ukosefu wa walimu, ambako waliopo ni tisa wakati wanafunzi wako 537 na mmoja ya walimu hao yuko masomoni hivyo kusababisha ufundishaji hafifu.
Akisoma risala kwa niaba ya wenzake, mwanafunzi Gwido Sarufu, alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa majengo ya shule hususani madarasa na ukosefu wa madawati na vitabu.
Katika mahafali hayo, Mbunge Mgimwa aliahidi kuchangia madawati 30, mbunge wa viti maalum Lediana Mng’ong’o mifuko mitano ya saruji na Myovela aliahidi kutoa kompyuta mbili kwa shule hiyo.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa