Home » » SERIKALI YASISITIZWA VITA VYA UJANGILI

SERIKALI YASISITIZWA VITA VYA UJANGILI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

SERIKALI imetakiwa kudhibiti ujangili kama ilivyo kwa uhalifu wa ujambazi ikiwa kweli kuna dhamira ya dhati kulinda wanyama wanaopotea kila mwaka hususani tembo na faru.
Wito huo umetolewa na Mratibu Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (Spanest), Godwell Ole Meing’ataki, wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya maandamano ya tembo na faru duniani, ambayo kimkoa yalifanyika mjini Iringa mwishoni mwa wiki.
Ole Meing’ataki, alisema ujangili wa tembo na faru haupaswi kufumbiwa macho na serikali, kwa kuwa wahusika wanajulikana na kuvitaka vyombo vya dola na Watanzania kwa ujumla kushirikiana katika kuwalinda kwa kuwafichua wote wanaojishughulisha na ujangili.
Alisema kuwa, wahusika wa ujangili ni Watanzania wenyewe, ndugu na majirani, hivyo kutokana na kuishi kwa umoja baadhi yawezekana wanajulikana katika jamii.
Ole Meing’ataki, alisema vijana walioko vijijini ambao mara nyingi ndio wanaohusika na uuaji wa tembo na faru, wanapaswa kupatiwa elimu kutambua madhara ya ujangili na kujua umuhimu wa maliasili ili ziwanufaishe wote.
Alisema kuwa, shirika la Spanest kwa kushirikiana na wadau wengine, wataendelea na utaratibu wa kutoa elimu vijijini ili maliasili hizo zilindwe kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Awali, Mratibu wa Maandamano hayo ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa shirika la Wildlife Connection, Julius Mbuta, alisema pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali katika kutokomeza ujangili, lakini mapambano yanapaswa kuhusisha wadau wote wakiwemo wananchi wa kawaida.
Kwa upande wake, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye pia ni Waziri Kivuli Maliasili na Utalii, alisema suala la kulinda maliasili ni la kila Mtanzania kwa mujibu wa Katiba na akawataka wananchi wote kushiriki kikamilifu kupambana na kuwafichua majangili wote.
Alisema maliasili zinakuza uchumi wa taifa na kwamba, mapambano dhidi ya ujangili hayapaswi kuchukuliwa kisiasa kwa kuwa yatadidimiza uchumi.
“Siasa haiwezi kutenganishwa na uchumi, maliasili hizi ndizo zinazokuza uchumi wetu kwa kuleta fedha nyingi za kigeni, leo hii kama tusingekuwa na tembo kamwe hawa Wazungu wasingeweza kuja kwetu, lazima tushikamane pamoja kuutokomeza ujangili,” alisema Msigwa.
Hata hivyo, pamoja na kuunga mkono jitihada za serikali katika kupambana na ujangili, alisema ni vyema elimu ikatolewa kwa Watanzania wote huku wananchi wa vijijini wakipewa kipaumbele, kwani ndio wahusika na washirika wakubwa.
Chanzo:tanzania daima

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa