Home » » CHADEMA WATAKA POLISI KUTENDA HAKI

CHADEMA WATAKA POLISI KUTENDA HAKI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Patrick Ole Sosopi na Mchungaji Msigwa wakihutubia Kihesa
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelitaka Jeshi la Polisi mkoani hapa kutenda haki kwa vyama vyote vya siasa katika kudhibiti misafara mirefu ya magari, pikipiki na aina yoyote ya maandamano tofauti na sasa wanaibeba CCM.
Juzi, Jeshi la Polisi liliwazuia wafuasi wa chama hicho Iringa Mjini kumlaki kwa maandamano ya magari na pikipiki, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA Taifa (Bavicha), Patrick Ole Sosopi aliyekuwa akiwasili akitokea jijini Dar es Salaam baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo.
Ole Sosopi na Mchungaji Msigwa, walipokelewa eneo la Igumbilo na viongozi na maelfu ya wafuasi wa chama hicho, lakini polisi mkoani hapa waliwazuia wafuasi hao kuwapokea kwa misafara ya magari na bodaboda.
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Sokoni Kata ya Kihesa, Mchungaji Msigwa, alisema watashangaa na kuchukua hatua endapo Polisi itairuhusu CCM kuwa na maandamano na misafara ya magari na pikipiki wakati wao wamezuiliwa kufanya hivyo wakati wa mapokezi ya Makamu Mwenyekiti Bavicha Taifa, Ole Sosopi.
Alisema kuwa CHADEMA itaingilia maandamano ya CCM Mkoa wa Iringa wakati wa mapokezi ya Katibu wake mkuu, Abdulrahman Kinana Oktoba 11 endapo yataambatana na misafara mirefu ya magari.
Mchungaji Msigwa, alikitaka Chama Cha Mapinduzi kuacha tabia ya kulitumia jeshi la polisi kuikandamiza CHADEMA pekee na huku wao wakifanya yale waliyozuiliwa CDM katika mikutano yake au maandamano.
“Jeshi la Polisi linatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi, liiache kufungamana na Chama Cha Mapinduzi kwa kuwabeba na utawala wowote ambao unatumia jeshi kutawala, fahamu kuwa wameishiwa hoja, kwa nini kila CHADEMA wakitaka kufanya jambo wanawakataza,”.
“CCM waliwahi sema kuwa hatuna watu, je kama hatuna watu kwanini wanakataza sisi tusiandamane? Leo vijana wametii maelekezo ya Polisi, vijana wetu wa bodaboda wamezuiwa kutupokea lakini wajue kuwa, Kinana akija hapa na maandamano hakutakalika,” alisema Msigwa huku akishangiliwa na maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Kwa upande wake, Ole Sosopi alisema kuyazuia maandamano ya CHADEMA na kuruhusu ya CCM, kutadhihirisha jinsi Polisi wanavyokibeba chama hicho tawala na kulitaka jeshi hilo kutenda haki kwa vyama vyote.
Alisema wakati wakijiandaa kuchukua dola, wanataka kuona wanashindana katika uwanja sawa wa kisiasa, kwa hiyo hawatakubali kuona jeshi la Polisi linaruhusu maandamano katika misafara ya Kinana wakati kwao linakataa.
Aidha, aliwataka vijana, wanawake na wazee wajitokeze kwenye daftari la ukazi ili kuwa wapigakura halali wakati uchaguzi za serikali za mitaa unaotarajia kufanyika Desemba 14 mwaka huu pamoja na ule mkuu wa 2015, kwa kuwa bila kufanya hivyo watakosa haki ya kuchaguliwa na kuchagua viongozi wanaowataka wakati chaguzi hizo na kuendelea kuiacha CCM kuendelea kutawala.
Akizungumzia Katiba iliyopendekezwa, Ole Sosopi alisema imechakachuliwa na CCM na kuwataka wananchi kuipinga mara itakapoletwa kwa wananchi kwa ajili ya kuipigia kura kwa kuwa itakuwa sio ya wananchi bali ya Chama Cha Mapinduzi.
“Kinana na Nape walaaniwe kwa kuwatembelea wananchi na kuwauliza wanataka katiba au maji, lakini hawakumbuki kuwazuia wabunge wao wakiongozwa na Sitta kuendelea na bunge maalum wakila mabilioni ya fedha na wao wakisema wananchi hawataki katiba,” alisema kuhoji.
Je kama wananchi hawataki katiba, kwanini bunge linaendelea wakati UKAWA wamejitoa katika mchakato huo hadi wanafikia hatua ya kupiga kura za kihuni za whatsup nk zinazovunja sheria za bunge hilo
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa