Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MBUNGE wa Kalenga mkoani Iringa Godfrey Mgimwa amewataka wazazi
kuacha tabia ya kuwapeleka watoto wao waliohitimu darasa la saba
kufanya kazi za ndani mijini kwa kuwa ni aibu kwa wakazi wa mkoa huo.
Akizungumza katika mahafali ya darasa la saba katika shule ya msingi
Kalenga na Kiponzelo juzi mbunge Mgimwa alisema kuwa mkoa wa Iringa
umekuwa ukisifika kwa kutoa wafanyakazi wa ndani jambo ambalo ni aibu
na asingependa jimbo lake kuwa katika orodha ya yanayosifika kwa hilo.
Mbunge huyo, alisema kwa muda ambao atakuwepo madarakani kama mbunge,
atafurahi kuona wazazi wanawasomesha watoto wao elimu ya Sekondari ama
ufundi ili kuja kuwasaidia mbeleni, badala ya kuwaruhusu kwenda mijini
kutumikishwa kazi za ndani na kwenye madanguro, ambako yanaweza
kuwasababishia kurudi kijijini na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
"Wazazi wa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba katika shule zote za
msingi jimbo langu la Kalenga, ninaomba sana kuungana katika kulijenga
jimbo kwa kutowaruhusu watu wenye nia mbaya kuja kukusanya watoto wetu
na kuwapeleka mijini katika kazi za ndani na madanguro," alisema.
Alisema kitendo cha baadhi ya wazazi kutopenda kuwasomesha watoto
elimu ya sekondari na kuwaruhusu kwenda kufanya kazi ya ndani si
heshima kwa Kalenga na mkoa mzima, bali ni aibu kubwa ambayo kama
isipo kemewa itajenga dhana ya kuwa Iringa ni kisima cha wafanyakazi wa
ndani.
Mgimwa alisema kuwa umefika wakati kwa wakazi wa Iringa kuungana
pamoja na kuugeuza mkoa huo kuwa wa maendeleo badala ya kuwa wa
kuzalisha wafanyakazi wa ndani.
Katika mafahali hayo, Mgimwa alijitolea kusaidia ujenzi wa choo cha
wanafunzi katika shule ya Msingi Kalenga kwa kutoa fedha za kununua
bati 43 pamoja na kusaidia ujenzi wa vyoo vya matundu 18 ya wanafunzi
katika shule ya msingi Kiponzelo.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment