Home » » MWIGULU ATAKA WAFANYABIASHARA WAKUBWA KUBANWA KWA KODI

MWIGULU ATAKA WAFANYABIASHARA WAKUBWA KUBANWA KWA KODI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Naibu Waziri wa Fedha,Mwigulu Nchemba.
 
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Bara ambae pia ni Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ameitaka serikali kuu na halmashauri zote nchini kuhakikisha wanawatoza kodi wafanyabiashara wakubwa badala kuwabana kodi wafanyabiashara wadogo na wananchi wenye kipato cja chini peke yao.
Alitoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mwembetogwa, Manispaa ya Iringa wakati wa sherehe ya kumsimika Kamanda wa Vijana wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM), Salim  Abri Asas.

Nchemba alisema njia ya kuondokana kuondokana na umasikini ni kuwatoza kodi wafanyabiashara wakubwa na kuwapatia huduma wananchi masikini.

“Katika serikali ya mitaa tunazounda mnatakiwa kuunda serikali ambayo itakuwa imeshikamana na ikiwa na lengo la kuwasaidia masikini na siyo viongozi,” alisema.

“Nataka niwaambie wakazi wa Iringa tumejiwekea utaratibu mzuri ambao tunataka kila mkoa ifanye ni kiwa na lengo la kusema kuwa tukusanye kodi kwa matajiri na kuwasaidia masikini, haiwezekani tukusanye kodi kwa masikini na akina mama wajane na kuwaongezea walionacho huku ni kuwakandamiza,” alisema Nchemba.

Kwa upande wake, Asas alisema vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo changamoto ya kiuchumi pamoja na ya kijamii.

Asas alisema kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo atawasaidia kadri atakavyoweza ili kuhakikisha vijana wanaondokana na majanga ya dawa za kulevya na pia aliwaahidi wakazi wa Iringa kuwatengenezea kituo cha kutibu vijana walioathirika na dawa za kulevya.

“Nitawasaidia pasipo kujali itikadi ya vyama dini wala kabila, ninajua kwamba vijana wote ni wetu na tutashirikiana katika kutatua matatizo hayo na ninaamini kwa kuwasaidia huko tutaongeza nguvu kazi ya Taifa ambayo ni vijana na kizazi kijacho,” alisema Asas.

Kwenyekliti wa CCM mkoa wa Iringa, Jesca Msambatavangu, alisema kuwa chama hicho bado kina jukumu la kulikomboa Jimbo la Iringa Mjini kutoka upinzani ambalo mbunge wake ni Mchungaji Peter Msigwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Msambatavangu alidai kuwa katika kipindi cha miaka minne ambacho Mchungaji Msigwa ameliongoza jimbo hilo,  limedhoofika kimaendeleo.

Hata hivyo, Msambatavangu hakueleza namna maendeleo yalivyofoofika zaidi ya kusema kuwa nguvu zote za Mchungaji Msigwa zimeelekezwa katika maandamano ya kila wakati.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa