Home » » MBOPIMA YAPIGWA TAFU MILIONI 60/-

MBOPIMA YAPIGWA TAFU MILIONI 60/-

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mbopima yapigwa tafu milioni 60/-JUMUIYA ya Matumizi Bora ya Mali Hai Tarafa ya Idodi na Pawaga mkoani Iringa (Mbomipa), imepewa msaada wa sh milioni 60 na kampuni ya Mkwawa Hunting Safaris ya mjini Iringa kwa ajili ya kuimarisha ulinzi dhidi ya ujangili katika eneo la hifadhi zinazoizunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.
Akikabidhi msaada huo hivi karibuni, Mkurugenzi wa Mkwawa Hunting Safaris, Ahmed Huwel, alisema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Mbomipa na wadau wengine katika kulipa ada na kuwasaidia pale ambako unahitajika msaada, ili kuhakikisha maliasili katika eneo hilo la hifadhi zinalindwa na kuvunwa kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na jumuiya hiyo na serikali.
Akipokea fedha hizo kwa niaba ya jumuiya hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Mbomipa, Juma Kaundama, aliipongeza kampuni hiyo kwa kujali na kutoa ushirikiano pale inapoombwa kufanya hivyo.
Alisema jukumu la ulinzi wa maliasili dhidi ya majangili, linagharimu kiasi kikubwa cha fedha na mara kwa mara kampuni ya Mkwawa imekuwa ikisaidia jumuiya hiyo katika kutekeleza majukumu yake.
Alibainisha kuwa, kuendesha jumuiya hiyo zinahitajika sh milioni 150 kila mwaka kwa ajili ya kununulia vifaa mbalimbali vikiwemo vya ulinzi, mikutano na gawio kwa vijiji vinavyounda jumuiya hiyo na mishahara.
Mbomipa ni jumuiya inayoshughulika na uhifadhi wa maeneo ya hifadhi ya wanyamapori ya jamii (WMA), nje ya mipaka ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wilayani Iringa. Wanyama walioko katika eneo hilo wanatoka ndani ya hifadhi hiyo na Hifadhi ya Mikumi
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa