Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba
amezitaka halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji kuongeza
mapato kwa kukusanya kodi za majengo badala ya kukimbizana na
wafanyabiashara ndogondogo na wajane.
Akizungumza na wananchi wa Manispaa ya Iringa
kwenye Uwanja wa Mwembetogwa baada ya kumsimika Salim Abri kuwa kamanda
wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Iringa, Nchemba alisema tabia ya
halmashauri na Serikali kushughulika na wafanyabiashara wadogo na
kuwaacha wakubwa wakiendelea kukwepa kodi, imepitwa na wakati.
“Naziagiza halmashauri nchini kuacha kukimbizana
na wajane wanaouza matembele (mboga za majani) na samaki wachache,
badala yake wakusanye kodi za majengo ambazo ni nyingi,” alisema.
Alisema duniani kote utaratibu ni kukusanya kodi
kubwa kwa matajiri ili kutoa huduma bora kwa maskini kwa kuwaboreshea
huduma mbalimbali.
Alisema kinachotakiwa ni kuwafichua wote wenye
majengo wanaokwepa kulipa kodi, jambo ambalo linawezekana kufanikiwa
zaidi kwa kuwapata viongozi bora kupitia Serikali za mitaa.
Vilevile alisema mpango wa Serikali hivi sasa ni
kupunguza matumizi na kuongeza mapato, ambapo wameanza na elimu kwa
kulipa mishahara kupitia kwenye akaunti za walimu moja kwa moja ili
kudhibiti mishahara hewa.
Aliwataka watumishi waliokuwa wanafuja fedha za umma kupitia mishahara hewa watafute kazi kwingine, kwani mwisho wao umewadia.
Aliwaonya watumishi wa umma kuacha matumizi mabaya
ya fedha za wananchi ilihali walipa kodi wakiwa na matatizo mengi
yanayohitaji kutatuliwa.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment