Home » » KAMATI TANO BUNGE LA KATIBA ZAKWAMA

KAMATI TANO BUNGE LA KATIBA ZAKWAMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mwenyekiti wa kamati namba tano, Steven Wasira
 
Kamati tano kati ya saba za Bunge Maalumu la Katiba zimejikuta katika njiapanda ya kushindwa kufanya maamuzi kutokana na kukosekana kwa akidi kwenye vikao vya kamati hizo.
Kwa mujibu wa mjumbe mmojawapo wa Bunge hilo, Teddy Ladislaus, kukosekana kwa akidi katika kamati nyingi kumezifanya zishindwe kufanya maamuzi  ikiwamo upigaji kura kwenye ibara mbalimbali.

Ladislaus, ambaye ni kutoka kundi la 201 akiwakilisha wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, alisema mjadala ndani ya kamati hizo umekuwa mgumu na kamati zinashindwa kumaliza kazi kwa muda uliopangwa kutokana na kukosekana kwa akidi ya kuwezesha kufanya maamuzi kutokana na wajumbe kutohudhuria kwa sababu mbalimbali.

Hadi sasa kati ya kamati saba zilizotoa maendeleo ya mjadala wa rasimu ya katiba ni kamati mbili pekee zilizopigwa kura katika kile kilichojadiliwa.

Mwenyekiti wa Kamati namba moja, Ummy Mwalimu, juzi aliahidi kuwa upigaji kura ungefanyika siku hiyo baada ya kujadili sura nne za rasimu hiyo, lakini hadi sasa zoezi hilo halijafanyika.

Aidha, Mwenyekiti wa kamati namba tano, Steven Wasira, akizungumza na NIPASHE alisema upigaji kura haujafanyika kwenye kamati yake licha ya kujadili sura ya pili, tatu, nne na tano.

Kamati zilizotoa mrejesho wa majadiliano yao hadi sasa ni namba 9, 10, 11, 12, ambazo hazijaeleza kama wamepiga kura, huku kamati namba tatu wakipiga kura na kuwa na maoni ya wengi na wachache.

ATAKA BUNGE LIAHIRISHWE
Katika hatua nyingine, Ladislaus alisema viongozi wakuu wanapaswa kutambua kuwa katiba bora itapatikana kwa maridhiano na siyo kwa ushindani na ubabe wa kisiasa.

Aidha, alisema vilevile kuwa ni vyema bunge hilo likaahirishwa kwa kuwa hivi sasa, kamati zinajadili sura za rasimu ya katiba kwa muundo wa "bora liende" na hakuna matumaini ya kupata katiba mpya yenye misingi ya umoja wa kitaifa.

Ladislaus aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa ni vyema Rais akaona umuhimu wa kusitisha shughuli za Bunge hilo kwa sasa na kutafuta maridhiano ya pande zinazovutana.

Mjumbe huyo, ambaye katika mkutano huo alikuwa ameambatana na Rais Mstaafu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Hemed Mngwali na Mwanafunzi wa Chuo cha Mipango Dodoma (ARDP), Elisante Mfinanga, alisema tamko analolitoa ni kwa niaba ya wanafunzi wa vyuo vikuu anaowawakilisha ndani ya bunge la katiba.

Alisema kuwa hadi sasa, Bunge hilo lipo katika mkwamo mkubwa kwani licha ya kamati kuendelea na uchambuzi wa rasimu, ukweli ni kwamba (wajumbe) wanapata ugumu kufikia akidi ya kuwezesha vikao kufanya maamuzi na kukidhi matakwa ya sheria ya mabadiliko ya katiba.

"Kamati za Bunge Maalum zinaendelea na uchambuzi wa Rasimu ya Katiba, lakini ni kweli kwamba uchambuzi huu wa sasa hauwezi kutuletea katiba bora inayokusudiwa na Rais Jakaya Kikwete... muda wa siku 16 kujadili sura 15 zenye ibara 240 ikiwa ni wastani wa ibara 16 kwa siku moja kazi haitafanyika kwa weledi," alisema.

Mjumbe huyo alitoa maoni yaliyoungwa na wenzake, akisema kuwa ni vyema Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania litakaloketi Novemba mwaka huu kufanya marekebisho kwenye katiba ya sasa ya mwaka 1977 kwa kuweka vipengele vya kuwapo kwa tume huru ya uchaguzi, haki ya kuhoji matokeo ya urais na kuwapo kwa mgombea binafsi.

Aliongeza kuwa, kuendelea kuharakisha mchakato wa kutengeneza Katiba kwa namna inayoendelea sasa hakutaleta katiba bora kwani haitakuwa na ridhaa ya makundi mengi kwenye jamii.

UGUMU KWENYE KAMATI
Ladislaus alibainisha kuwa kwa kadri anavyoona, hivi sasa kamati za Bunge Maalum la Katiba zimekuwa zikifanya kazi alimradi tu kufika mwisho na ionekane kwamba kazi ya kupata katiba mpya imefanyika, jambo analoamini kuwa ni dhambi kubwa kwani kufanya hivyo ni kuhadaa mamilioni ya Watanzania kuwa watapatiwa katiba bora wakati hilo halitawezekana bila pande zote zinazovutana kufikia maridhiano.

"Kwa kuwa Katiba ni moyo wa nchi, tusifanye kazi kwa kulipua alimradi tuwapendeze wachache walioweka maslahi binafsi mbele.Tukifanya hivyo tutakuwa tunaliweka taifa rehani ... na baadaye taifa litaachwa liharibike mikononi mwetu sisi vijana," alisema. Akielezea kuhusu haja ya kuwapo kwa mazungumzo baina ya CCM na Ukawa, Ladislaus alisema:

"Mazunguzo siku zote ni 'give and take' yaani kulegeza msimamo katika baadhi ya hoja badala ya kila upande kushupaa kwa kile unachokiamini, tukiwa na nia ya dhati ya kuzungumza, tukashauriana, tukaridhiana na kukubaliana jinsi ya kutekeleza yale tulioafikiana, basi Taifa litapata Katiba bora hivyo kuondoka katika mkwamo wa sasa na kuondoa mgawanyiko," alisema.

Ukawa huundwa na wajumbe kutoka vyama vikuu vya upinzani nchini vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.

Wajumbe wa Ukawa walisusia vikao vya Bunge Maalum la Katiba tangu April 16, 2014, ikiwa zimebaki siku 10 Bunge hilo kuhairishwa na wameweka msimamo wa kutorejea tena Bungeni hadi litakapojikita kwenye kujadili Rasimu ya wananchi iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Imeandikwa na Salome Kitomari, Editha Majura na Godfrey Mushi, Dodoma
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Powered by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Iringa Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa