Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Jina la Madaraka Kilangi (52) kwa wenye malori makubwa aina ya Scania Kanda ya Nyanda za Juu Kusini lipo mdomoni.
Ni fundi na muuzaji maarufu wa vipuri vya magari hayo kwa miaka 30, ni mtu mwenye historia fupi, lakini yenye kuvutia.
Kilangi mwenye elimu ya darasa la saba aliyoipata
katika Shule ya Msingi Mwembetogwa mjini Iringa, kwa sasa ni mfanyakazi
na mmiliki wa kampuni tatu zenye majina makubwa jijini Mbeya.
Anamiliki Kampuni za Madaraka Auto Garage, Lulu
Auto Spares na Mbeya Spring drinking Water and Kilangi Investiment
Company Limited. “Mimi nina elimu ya darasa la saba, Mungu amenipa
madaraka ya kuthubutu na hatimaye kumiliki mali ingawa siyo tajiri,
kwani mbali ya kampuni zangu, pia ninamiliki nyumba 10 za kupangisha na
magari mawili ya kunyanyua magari mazito yaliyoanguka,’’ anasema.
Kilangi akiwa amevalia koti la bluu la kikazi
zaidi akiwa katika gereji yake, anasema siri ya mafanikio yake ni
kujituma na uaminifu.
“Baada ya kumaliza elimu ya msingi niliomba
kibarua kwenye Kampuni ya Maliki Auto Garage na pale nilifanya kazi kwa
bidii na kujifunza mambo mengi,’’ anasema Kilangi.
Anasema baada ya miaka 14 kwenye gereji hiyo,
alinunua kiwanja kwa Sh100,000 na kuanzisha gereji yake ndogo ambayo
aliipa jina la Madaraka Auto Garage.
“Hapa nilikuwa na vijana niliowafundisha kazi na
wengi wao kwa sasa wana gereji kubwa katika Jiji la Dar es Salaam,
Iringa na hata hapa Mbeya,’’ anasema.
Kilangi mwenye wake wawili, anasema baada ya muda
alifungua duka la kuuza vipuri vya magari aina ya Scania pekee. “Mimi
naamini umasikini ni matokeo ya uoga katika kuthubutu, kwani mimi
nilithubutu kukopa fedha nyingi benki licha ya riba kuwa kubwa, lakini
walau nilipata mtaji ambao nazunguka nao mpaka sasa.’’
Anatoa mfano wa riba kuwa kubwa kwamba mtu akikopa
Sh200 milioni benki atarudisha jumla ya Sh350 milioni, ikiwamo riba ya
Sh150 milioni. Kilangi anasisitiza umuhimu wa mtu anayekopa kuwa na
malengo ili aweze kufanikiwa na kusema hofu yake kwa sasa ni mtazamo
mbaya wa vijana wanaomaliza vyuo vikuu wanapotafuta kazi.
“Pamoja na kwamba mimi ni mkurugenzi mkuu, lakini
nauza duka langu, nashika spana na kuhangaika na kazi zote za kampuni.
Nashindwa kuwaamini vijana wanaohitimu vyuo vikuu hapa nchini, kwa
sababu hawatabiriki. Hawana ari na kazi, wanafikiria zaidi kuiba tofauti
na vijana wasomi kutoka Zambia, Kenya au Uganda ambao wakipata kazi
wanafanya kwa bidii,’’ anasema.
Itaendelea Alhamisi ijayo
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment