Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, Evarista Kalalu,
amewataka wananchi wa wilaya hiyo kujenga tabia ya kupanda miti na
kutunza mazingira kwa lengo la kukabiliana na changamoto za mabadiliko
ya tabia nchi yanayoendelea duniani kote.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Umoja wa Vikundi vya Kijamii
Mufindi (Uvikimu) unaojihusisha na uoteshaji wa miche ya mbao na
matunda, ufugaji wa nyuki, pamoja na ufugaji wa kuku, Kalalu alisema
upungufu wa mvua kwa baadhi ya maeneo ni matokeo ya kudharau ushauri
huo ambao hutolewa kila mara kwa wananchi.
Kalalu alipongeza hatua ya Uvikimu na kusema ni hatua muhimu kwa
wanajamii wote kutambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira, ili kuendelea
kunusuru maisha ya viumbe hai na mmomonyoko wa udongo.
Ofisa Maendeleo ya Vijana Wilaya ya Mufindi, Juma Fuluge, alisema
uelewa mdogo wa wananchi kushindwa kujiunga na vikundi mbalimbali vya
ujasiriamali ni jambo linalorudisha nyuma maendeleo, hivyo kuwataka
wananchi kujitokeza kwa wingi kujiunga katika vikundi hivyo, ili
waweze kujikwamua kiuchumi.
Baadhi ya wajasiriamali wameendelea kulia na ukosefu wa mitaji na
masoko ya kuuzia bidhaa zao na kuomba serikali kuwaangalia kwa jicho la
huruma.
Uvikimu imeanzishwa mwaka juzi na hadi sasa ina wanachama 770 kutoka katika vikundi 35.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment